Ligi Kuu Bara yarejea rasmi

22May 2020
Romana Mallya
Dodoma
Nipashe
Ligi Kuu Bara yarejea rasmi
  • Rais Magufuli atangaza michezo yote kufanyika kuanzia Juni Mosi, lakini mashabiki

KIPENGA kimelia! RAIS John Pombe Magufuli ametangaza rasmi kufungua michezo yote nchini kuanzia Juni Mosi, mwaka huu lakini amesisitiza taratibu za mashabiki kushangilia zitatolewa kitaalamu na wizara husika.

Rais John Magufuli, akizungumza na viongozi aliowaapisha katika Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma jana. PICHA: IKULU

Rais Magufuli alitoa maagizo hayo jana katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni.

Magufuli alisema wizara zitakazotoa mwongozo wa namna ya kuruhusu mashabiki ni Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

“Kuna michezo ya jeshi, ni lazima watu wafanye michezo, taratibu za kushangilia na kuangalia zinaweza kupangwa vizuri na Wizara ya Afya pamoja na wizara husika ya michezo ili ule umbali kati ya mtu na mtu ukaendelea kuwapo katika kipindi hiki cha maambukizi,” Magufuli alisema.

Alisema kutokana na maambukizi ya virusi vya corona kupungua hapa nchini, ameamua kufungua michezo kwa sababu anafahamu kila mtu anaipenda.

“Ninafahamu kila mmoja anapenda michezo hata wabunge wanakwenda kwenye michezo, katika mwenendo niliouona, sina hakika kama kuna mwanamichezo aliyefariki hapa Tanzania kwa corona, kuwa na michezo kunasaidia kupambana na corona.

“Kuwa na michezo kunasaidia kupambana na corona na michezo ipo mingi, kila mmoja na mchezo wake, lakini michezo ni kitu kinachosaidia.

Kiongozi huyo aliongeza michezo ipo ya aina mbalimbali ikiwamo sanaa ya kuigiza, na uamuzi wa kujibana kwa kiwango cha juu si salama.

"Si lazima tusijibane sana, kukutana kutana huku kunajenga kinga za mwili hii, na hii itatusaidia kupambana na magonjwa, na si corona tu, hata na magonjwa mengine itatusaidia,” aliongeza Magufuli.

Alisema pia ukifungia watu katika nyumba kwa siku nyingi, siku utakayowafunguliwa, kinga zao za mwili zitakuwa zimeshuka kwa asilimia 30.

"Nataka kuwahakikishia Tanzania tunaenda vizuri, tuko vizuri, na Mungu wetu ameendelea kutusimamia, tulianza na Mungu, nina hakika tutamaliza na Mungu, hakuna mahali popote taifa lililomtegemea Mungu likaenda kushindwa,... Mungu amejibu, amejibu maombi yetu, amejibu kwa kiasi kikubwa na amejibu kwa kishindo," alisema Magufuli.

Machi 17, mwaka huu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alitangaza kusitisha mikusanyiko yote ikiwamo shughuli za michezo na matamasha ya muziki.

Habari Kubwa