Ligi Kuu Z'bar kuendelea Feb 5

06Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Zanzibar
Nipashe Jumapili
Ligi Kuu Z'bar kuendelea Feb 5

CHAMA cha Soka Zanzibar (ZFA) kimetangaza kusimamisha ligi mbalimbali ili kupisha mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayoendelea visiwani hapa yachezwe kwa ufanisi zaidi.

Mchezo wa kombe la Mapinduzi kati ya Azam na Jamhuri uwanja wa Aman Zanzibar

Katibu wa Kamati ya Mashindano ya ZFA, Alawi Haidar Foum, alitaja ligi ambazo zimesimama kupisha mashindano hayo ni pamoja na Ligi Daraja la Kwanza ambayo inakwenda mapumziko huku timu zote zikiwa zimecheza mechi 13 na Ligi Daraja la Pili ambayo inachezwa kwa mfumo wa makundi.

Foum alisema kuwa mechi za Ligi Kuu Zanzibar ambayo ilisimama tangu Januari Mosi itaendelea tena kuanzia Februari 5 mwaka huku dirisha dogo la usajili likiwa limefunguliwa na litamalizika ififako Januari 25 mwaka huu.

"Baada ya muda huo kumalizika, kamati husika ya ZFA itakutana ili kuangalia taratibu zilizofuatwa katika usajili huo na kutoa baraka kwa wale ambao watakuwa wamekamilisha mchakato huo," alisema kiongozi huyo.

Alizikumbusha klabu kuwa ZFA haitabadilisha kalenda yake na vile vile haitaongeza siku za kufanya usajili wa dirisha dogo, hivyo klabu zijipange kukamilisha mchakato huo.

Wakati huo huo Foum alisema kuwa mashindano ya Kombe la FA yatachezwa kwa mfumo wa mtoano ili kupata timu nne kutoka Pemba na nyingine nne za Unguja ambazo zitatinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Habari Kubwa