Ligi Zanzibar yarudi tena leo

14May 2022
Hawa Abdallah
ZANZIBAR
Nipashe
Ligi Zanzibar yarudi tena leo

LIGI KUU ya Zanzibar inaendelea leo Jumamosi baada ya kusimama kwa muda wa mwezi mmoja kupisha mfungo wa Ramadhani.

Ligi hiyo imebakiza michezo mitano kumalizika huku timu ya KMKM ikipewa nafasi kubwa ya kulinyakua taji hilo msimu huu.

Timu zitakazoshuka daraja tayari zimejulikana ambazo kutoka Kanda ya Pemba ni Yosso boys, Machomane, Kisiwani na Selem View.

Aidha kwa leo kutakuwa na michezo miwili ambapo katika dimba la Amaan, Polisi watawakaribisha KVZ majira ya saa 10:00 Alasiri.

Wakati majira ya saa moja 1:00 usiku Uhamiaji watawakaribisha KMKM katika uwanja wa Amaan.

Akizungumza na gazeti hili, Kocha wa timu ya KMKM, Ame Msimu alisema matarajio yake ni kuona wanashinda mchezo huo ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kutwaa ubingwa.

Alisema KMKM katika michezo mitano iliyobaki anatakiwa ashinde miwili ili kutwaa taji hilo msimu huu.

Alisema kuwa alama sita ni ndogo, lakini ni nyingi kuzitafuta kutokana na kuwa kila timu katika michezo hii ya mwisho inahitaji kushinda.

Hata hivyo, aliwataka mashabiki wa KMKM kujitokeza kwa wingi uwanjani katika michezo ya mwisho ili kuwapa hamasa.

Timu ya KMKM ambao ndio vinara wa ligi hiyo wana alama 57 huku wapinzani wao JKU wana alama 47 huku nafasi ya tatu ikishikiliwa na KVZ wenye alama 45.

Habari Kubwa