Lipuli Day kufanyika kesho Iringa

25Oct 2020
WAANDISHI WETU
Iringa
Nipashe Jumapili
Lipuli Day kufanyika kesho Iringa

UONGOZI wa Lipuli unatarajia kutambulisha rasmi jezi yake mpya watakayoitumia katika msimu wa 2020/21 wa Ligi Daraja la Kwanza kwenye tamasha la klabu hiyo "Lipuli Day" litakalofanyika kesho kwenye Uwanja wa CCM Samora mkoani hapa.

Mwenyekiti wa Lipuli, Ayubu Kiwele, alisema maandalizi ya tamasha hilo yamekamilika na wanawaomba mashabiki na wadau wa soka wa Iringa kujitokeza kuangalia mikakati iliyopangwa na klabu yao.

Kiwele alisema wanaishukuru Kampuni ya Vunjabei ambayo ilikubali kuingia udhamini wa mwaka mmoja, ambao utawafanya wapate vifaa mbalimbali vya michezo ikiwamo jezi.

"Tumejipanga kufanya vizuri katika Ligi Daraja la Kwanza, hatutaki kurudia makosa, tunaahidi tutarejea tena Ligi Kuu Bara msimu ujao," alisema kiongozi huyo.

Kiwele alisema kampuni hiyo pia itauza jezi za timu yao katika maduka yake yote na klabu itapata mgawo wake kulingana na makubaliano ambayo wamefikia.

Naye Meneja wa Kampuni ya VunjaBei, Fadhili Ngajilo, aliishukuru klabu hiyo kwa kukubali kushirikiana nao na wameahidi kuisaidia ili irejee katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

"Tumesaini mkataba wa mwaka mmoja na Kampuni ya Vunjabei, mkataba huo unahusisha pia kuuza jezi za Lipuli. Zinapatikana kwa Sh. 20,000. Kwa Iringa duka lipo Uhindini. Timu hiyo tumeidhamini kwa kuipa vifaa na jezi kwa msimu wote wa ligi," alisema Ngajilo.

Kabla ya kushuka daraja, iliichukua miaka 17 kwa Lipuli kurejea tena katika Ligi Kuu Bara ambayo bingwa wake hushiriki mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mbali na Lipuli, timu nyingine kutoka Ligi Kuu Bara zilizoshuka daraja ni pamoja na Singida United, Alliance FC, Ndanda FC na Mbao FC.

Habari Kubwa