Lule apania kuipeleka Mbeya City kimataifa

18May 2022
Saada Akida
Nipashe
Lule apania kuipeleka Mbeya City kimataifa

KOCHA Mkuu wa Mbeya City, Mathias Lule, amepiga hesabu za kuibuka na pointi tatu dhidi ya KMC FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lengo lake likiwa ni kuongeza presha ya kuwania nafasi nne za juu kwenye ligi hiyo.

KOCHA Mkuu wa Mbeya City, Mathias Lule.

Mbeya City ambayo imeshuka dimbani mara 24, ipo nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 32 sawa na Azam FC iliyopo nafasi ya tatu baada ya kucheza mechi 23.

Timu hizo zinazidiwa pointi mbili na Geita Gold FC iliyopo nafasi ya tatu baada ya kushuka dimbani mara 24 kwenye ligi hiyo ambayo Yanga ipo kileleni ikiwa na pointi 60, 11 zaidi ya Simba iliyopo nafasi ya pili.

Kikosi cha Mbeya City tayari kimewasili Dar es Salaam tangu jana na kesho kitashuka Uwanja wa Uhuru kuwavaa wenyeji wao, KMC FC.

Akizungumza na gazeti hili jana, baada ya mazoezi waliyofanya katika Uwanja wa Uhuru, Lule alisema wamejiandaa vizuri na mchezo huo kuhakikisha wanatafuta pointi tatu muhimu.

Alisema wachezaji walikuwapo katika safari yao wote wako fiti na tayari kwa ajili ya kutafuta pointi tatu zitakazowaweka katika mazingira mazuri ya kumaliza msimu wakiwa nafasi  nne ya msimamo wa ligi hiyo.

“Tumekuja kutafuta pointi muhimu katika mchezo wetu dhidi ya KMC FC, mechi itakuwa ya ushindani mkubwa kwa sababu tunahitaji alama tatu ili kujiweka katika malengo yetu na wapinzani wetu wanahitaji kutumia vizuri uwanja wao wa nyumbani kutafuta ushindi,” alisema Lule.

Alisema ligi imekuwa na ushindani mkubwa kwa sababu kuanzia nafasi ya tatu hakuna mwenye uhakika wa kudumu katika nafasi hiyo kwa sasa.

“Tunapoenda kucheza mechi yoyote malengo ya kwanza ni kushinda iwe nyumbani au ugenini, ili kujihakikishia nafasi tuliyopo au kupanda juu katika msimamo,” alisema kocha huyo ambaye amedhamiria kuiona timu hiyo inacheza michuano ya kimataifa msimu ujao.

Habari Kubwa