Lwandamina aikubali Simba

12Jan 2017
Faustine Feliciane
Nipashe
Lwandamina aikubali Simba
  • *** Asema kuna matumaini makubwa Ligi Kuu Bara kwani amepania...

KOCHA wa Yanga, George Lwandamina, amesema licha ya kutolewa hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi na Simba, bado ana nafasi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza na Nipashe jana muda mfupi baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam, Lwandamina, alisema amekubali matokeo aliyoyapata kwenye mchezo wa nusu fainali dhidi ya Simba kwa kuwa wapinzani wao waliitumia vema mikwaju ya penalti.

Kocha huyo, alisema anashukuru michuano hiyo ya mapinduzi imempa mazoezi ya kutosha kuelekea mechi za Ligi Kuu pamoja na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

"Tulikuwa na lengo la kuchukua ubingwa wa Mapinduzi, lakini mambo hayakwenda vile tulivyopanga, pamoja na hayo kipo tulichofaidika nacho, kwa mechi tulizocheza timu imepata mazoezi ya kutosha," alisema Lwandamina.

Alisema baada ya mapumziko ya siku moja timu itaanza mazoezi kujiandaa na mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Majimaji ya Songea watakayocheza nayo ugenini.

Aidha, Lwandamina amewataka mashabiki wa Yanga kutovunjika moyo kwa kuwa bado lipo kombe wanaloliwania na wanauwezo wa kulitwaa.

Katika hatua nyingine, Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh aliliambia Nipashe kuwa bado hawajajua mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Majimaji utachezwa lini.

Alisema baada ya ligi kusimamishwa kupisha mashindano ya Kombe la Mapinduzi bado hawajapewa taarifa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ni lini wanacheza mchezo wao huo.

"Tutaendelea na maandalizi yetu huku tukisubiri maelekezo ya TFF juu ya michezo yetu baada ya kumalizika kwa Kombe la Mapinduzi," alisema Saleh.

Habari Kubwa