Lwanga: Simba itafunika tena msimu ujao

27Jul 2021
Saada Akida
Kigoma
Nipashe
Lwanga: Simba itafunika tena msimu ujao

KIUNGO mkabaji wa Simba, Taddeo Lwanga amekiangalia kikosi cha timu hiyo na kudai kwamba bado wataendelea kutesa kutokana na ubora walionao kwa msimu ujao.

Mfungaji huyo wa bao pekee lililoipa Simba ubingwa wa kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (FA), Lwanga, alisema mafanikio yao msimu huu yametokana na ushirikiano wa wachezaji, benchi la ufundi, viongozi hadi mashabiki hali hiyo anatarajia kuwepo ndani ya klabu hiyo.

Raia huyo wa Uganda alisema Simba ni bora kuanzia kikosi hadi uongozi ikilinganishwa na watani wao Yanga, hivyo anaiona ikiendelea kutawala soka la Tanzania hadi Afrika kwa siku za usoni.

"Nikiangalia kikosi cha Simba naona kitaendelea kutawala soka la Tanzania kutokana na ushirikiano mzuri ndani ya klabu hii,” alisema.

"Ni kweli tumechukuwa ubingwa kwa kuwafunga Yanga ikiwa pungufu na kushinda bao 1-0 kwamba wapinzani wao ni wagumu, haijalishi hilo kwa sababu Simba ni Bingwa wa ligi na hii FA, tena mfululizo," alisema Lwanga.