Lyanga aingia rada za Yanga

26Apr 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Lyanga aingia rada za Yanga

WAKATI klabu ikiwa katika mchakato wa maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika ifikapo Mei 5, mwaka huu, Kamati ya Usajili ya Yanga imeanza mazungumzo na Coastal Union ili kumsajili mshambuliaji wa timu hiyo ya jijini Tanga, Ayoub Lyanga.

Ayoub Lyanga.

Akizungumza na gazeti hili jana, mmoja wa viongozi wa Coastal Union ( jina tunalihifadhi), alisema klabu yao iko tayari kumuuza endapo Yanga itatoa kiasi cha fedha walichowaambia.

Kiongozi huyo alisema kuwa awali Yanga ilianza kuzungumza na mchezaji huyo, lakini baada ya kubaini kwamba bado ana mkataba na Coastal Union walilazimika kufuata utaratibu sahihi wa usajili.

"Yanga wanatusumbua sana kuhusu Lyanga, ila tumewaambia watupe pesa tu, maana kama washaona atawafaa, sisi tutawauzia na tutaendelea kutengeneza vijana wengine," alisema kiongozi huyo aliyepo ngazi za juu Coastal Union.

Alisema klabu yake inajivunia kutumia zaidi wachezaji vijana inaowapandisha kutoka katika kikosi cha pili na wamekuwa wakiwapa matokeo mazuri licha ya kukabiliana na changamoto mbalimbali kutoka kwa timu pinzani.

"Coastal Union bado inaamini vijana ndio wenye uwezo na watakaosaidia kufanya mapinduzi ya kupunguza nyota wa kigeni wanaokuja kubahatisha, timu yetu ina wachezaji wengi wa U-20, wanafanya vema na wanawasumbua hao wanaojiita wakongwe," aliongeza kiongozi huyo.

Hata hivyo, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, alinukuliwa mapema wiki hii akikataa kuanza mchakato wa usajili kwa madai kwamba klabu hiyo haina fedha kwa sasa.

Lakini kamati ya kuchangisha fedha iliyoko chini ya Mwenyekiti wake, Anthony Mavunde, inaelezwa kuwa na zaidi ya Sh. milioni 500 baada ya kukusanya pesa kupitia harambee waliyoifanya mapema mwezi huu jijini Dodoma kwa kuwaalika viongozi mbalimbali wanaoipenda klabu hiyo.

Habari Kubwa