Mabeyo azindua uwanja wa gofu wa kimataifa

29Jun 2022
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Mabeyo azindua uwanja wa gofu wa kimataifa

MKUU wa Jeshi la Ulinzi nchini, Jenerali Venance Mabeyo amesema uwanja wa gofu unaojengwa katika eneo la Ihumwa jijini Dodoma ni wa viwango vya Olimpiki, hivyo utasaidia kuvutia michezo ya kimataifa kufanyika hapa nchini hapo baadae.

MKUU wa Majeshi Jenerali, Venance Mabeyo akipiga mpira wa Gofu kama ishara ya uzinduzi wa uwanja wa Gofu unaojengwa eneo la Ihumwa jijini Dodoma. PICHA NA RENATHA MSUNGU

Mabeyo alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa Uwanja wa gofu ambao umebeba viwanja vya michezo mbalimbali ndani yake uliofanyika jana eneo la Ihumwa jijini Dodoma.

Mabeyo alisema uwanja huo ni wa kwanza kujengwa jijini hapa lakini ni wa pili wa mchezo wa Gofu kujengwa na jeshi hilo hapa nchini, ambapo wa kwanza ni ule uliopo Lugalo, Dar es Salaam.

Alisema lengo la kujenga viwanja vya michezo ni pamoja na kuisapoti serikali katika kuendeleza michezo hapa nchini, ili watanzania wazidi kuipenda michezo pamoja na kupanua wigo wa kushiriki mashindano ya kimataifa.

“Naomba niipongeze kamati ya Ujenzi wa uwanja huu iliyo chini ya Mwenyekiti Brigedia Hassan Mabena imefanya kazi nzuri ya ubunifu wa uwanja huo,”alisema Jenerali Mabeyo.

Naye Jenerali Mstaafu wa Jeshi hilo, George Waitara aliwataka Majenerali kujifunza kucheza gofu ili watumie uwanja huo badala ya kutumika na wageni pekee.

Alisema gofu ni mchezo wa kila mtu na kuitaka jamii kujitokeza kwa wingi kushiriki mchezo huo na kuachana na dhana ya kudhani mchezo huo unachezwa na matajiri pekee.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Gofu nchini (TGU), Chris Martine aliwashukuru Jeshi hilo kwa kusapoti michezo hapa nchini,hususani mchezo wa Gofu kwa kuendelea kujenga viwanja vya mchezo huo na michezo mingine.

Habari Kubwa