Mabondia JKT, Ngome kukinukisha Dar

22May 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR
Nipashe
Mabondia JKT, Ngome kukinukisha Dar

Pambano kali la ngumi za kulipwa na ridhaa litakaloshirikisha mabondia mbalimbali nchini wakiwamo wa Jeshi la Kujenga Taifa na Ngome linatarajiwa kupigwa Juni 7, mwaka huu, katika Ukumbi wa Club 361 Mwenge Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mratibu wa Ufundi wa pambano hilo, Yassin Abdalah Ustaadh, alisema upinzani wa JKT na Ngome ni wa kihistoria na kuwataka mashabiki na wapenzi wa ngumi kujitokeza kwa wingi kuweza kushuhudia mpambano huo.

 “Mabondi wazuri wa ngumi za kulipwa ni wale walioanzia ngumi za ridhaa na kuwapo kwa JKT na Ngome katika pambano hilo ni hatua muhimu na mchango mkubwa wa jeshi katika kuendeleleza ngumi na michezo kwa ujumla,” alisema Ustaadh.

 Aliwataka mabondia wa ngumi za kulipwa watakaopanda ulingoni siku hiyo kuwa ni Nassib Ramadhani atakayezichapa na Mohamed Kashinde, wakati Kiasi Ally akinyukana na Shadrack Ignas, huku Kudura Tamimu akitoana jasho na Baina Mazola.

Alisema pambano lingine la kuvutia lenye lengo la kuvunja historia ya Japhet Kaseba kumkaribisha katika ngumi, mchezaji wa ngumi na mateke, Jeremia Jackson atakayecheza na Hashim Masungo.

 Kwa upande wa Kocha wa Ngome, Hassan Mzonge, alisema wamejiandaa vema na mmoja wa mabondi watakaopambana katika uzito wa kilo 81 ni Koplo Selemani Kidunda na kutuma salamu kwa JKT.

Kwa upande wake Katibu wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa nchini, Yahaya Poli, aliwapongeza waandaaji kutekeleza sera ya kamisheni kuchanganya mapambano ya kulipwa na ridhaa na kufafanua kuwa tayari kibali kimetolewa kwa ajili ya kufanyika kwa pambano hilo.

Nao wadhamini wa pambano hilo, Kampuni ya Euromax kupitia kwa Ofisa Masoko wake, Forgiver Tito, aliwaahidi wapenzi wa ngumi kuwa wataendelea kusaidia kukuza mchezo huo kwani ni sehemu ya ajira na kuwataka wadhamini wengine kujitokeza.

Naye Mratibu wa pambano hilo, Beatrice Ntahona, alisema maandalizi yote yamekamilika na watakahikisha kunapatikana ulingo mzuri na mandhari itakuwa nzuri kuhakikisha mabondia wanacheza vizuri na kupatikana mshindi halali.

Habari Kubwa