Magufuli amuahidi Diamond mubashara

15Mar 2017
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Magufuli amuahidi Diamond mubashara

RAIS John Magufuli, amesikia kilio cha wasanii wa kizazi kipya kuhusu wizi wa kazi zao na kuahidi kulifanyia kazi suala hilo.

rais john magufuli.

Magufuli alitoa ahadi hiyo jana asubuhi baada ya kupiga simu kwenye kituo kimoja cha Runinga wakati msanii wa kizazi kipya, Diamond Platinum akifanyiwa mahojiano mubashara.

Wakati mahojiano hayo yakiendelea, Diamond alitoa malalamiko dhidi ya kazi za wasanii na kumuomba Rais Magufuli afanyie kazi suala hilo kwa haraka kama anavyofanya kwenye mambo mengine, hata hivyo katikati ya mahojiano hayo Rais alipiga simu na kueleza kuwa, amesikia kilio hicho na kuahidi kulifanyia kazi suala hilo.

Akizungumza kwa njia ya simu, Rais Magufuli alisema, “Nimemsikia Diamond maombi yake na nimeyapokea, nimemfurahia yeye kusema ni CCM na kweli alishiriki kwenye kampeni, na wasanii wengine walishiriki kwa kweli nasema tu kwamba maombi yake nimeyasikia na nitapanga muda siku moja ili tukutane nao tuangalie namna nzuri ya kuwasaidia, nawashukuru sana nawatakia kipindi chema.

“Nawapongeza endeleeni hivyo, ninawaangalia live (Mubashara) na hongera Diamond na huwa nasikiliza nyimbo zako,” alisema.
Hata hivyo, Magufuli alimpongeza Diamond kwa kupata mtoto wa pili.

Naye Diamond alimweleza Rais kuwa, “Nashukuru sana nakuomba utusaidie sana, tunaamini wewe ni rais unayetetea wanyonge na sisi ni wanyonge, tunafamilia na watoto, tunategemea muziki ili tuweze kujiajiri na kuliingizia pato taifa.

“Ukiwekwa utaratibu mnzuri utakaowezesha kulipa kodi, sisi tupo tayari kulipa kodi, kama mimi ni mlipa kodi mzuri,” alisema Diamond.

Baada ya maelezo hayo, Rais Magufuli alimpongeza msanii huyo kwa kuitangaza Tanzania katika masuala ya muzuki na kueleza kuwa anawapenda wote hata waigizaji.

Aidha, Diamond alimshukuru Rais mstaafu wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Kikwete kwa kuwasaidia wasanii kuwawekea ‘stika’ kwenye kazi zao.

Habari Kubwa