Majaliwa awapigia magoti wadhamini

19Feb 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe
Majaliwa awapigia magoti wadhamini

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameyataka makampuni na taasisi mbalimbali kuidhamini michezo mingine, badala ya kuwekeza nguvu nyingi kudhamini mchezo wa soka peke yake.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Waziri Majaliwa alisema hayo juzi katika kikao cha pamoja kilichowahusisha pia viongozi wa vyama vya michezo kilichofanyika juzi kwenye Ukumbi wa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Aliwaambia kuwa kama kila kampuni itajikita kudhamini mchezo mmoja, anaamini mchezo husika utaendelea na kampuni au taasisi hiyo pia itapata nafasi ya kujitangaza kupitia mafanikio ya wanamichezo waliowadhamini.

"Hapa kama kila kampuni moja ikachagua mchezo mmoja na kuudhamini, nina hakika michezo yote ingekuwa inafanya vizuri, hata judo unaweza kukutangaza vizuri, mnatakiwa mpanue wigo," alisema Majaliwa.

Aliyataka makampuni na taasisi hizo kudhamini kuanzia ngazi ya wilaya ambayo ndiyo wanamichezo wanaandaliwa na kuacha tabia ya kusubiri timu zinapofika hatua ya kitaifa.

"Tunawaomba mdhamini vituo na kambi za timu za Taifa, vilevile tunawaomba msaidie kuanzisha vituo," alisema.
Aliongeza kuwa ili mafanikio yapatikane haraka ni vyema uwekezaji wa mafunzo ya makocha na warefa uimarishwe.

KODI
Waziri Mkuu huyo alisema ofisi yake inaendelea na mazungumzo na Mamlaka ya Kodi Nchini (TRA) kuhusiana na msamaha wa vifaa vya michezo, lakini itakuwa makini kuhakikisha vifaa vitakavyosamehewa ni vile ambavyo vimeletwa kwa matumizi ya wanamichezo tu.

"Hatuwezi kutoa kodi kwa vifaa vya mtu binafsi, hatutakubali mgongo wa serikali utumike," aliongeza.

Pia kiongozi huyo alipongeza uteuzi wa kocha mkuu mpya wa timu ya Taifa ya soka ya Wanawake (Twiga Stars), Nasra Mohammed na kueleza kwamba hiyo ni hatua nzuri.