Majimaji waanza kuifanyia kazi Yanga

05Jan 2017
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Majimaji waanza kuifanyia kazi Yanga

WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imesimama kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi, Kocha wa Majimaji ya Songea, Kally Ongala, amesema katika kipindi hiki timu yake itacheza michezo miwili ya kirafiki kujiandaa kwa mechi ijayo dhidi ya Yanga.

Kocha wa Majimaji ya Songea, Kally Ongala.

Akizungumza na Nipashe jana, Ongala, alisema kwa sasa wanaendelea na programu yao ya mazoezi ya kila siku, lakini watacheza michezo miwili na timu za mkoani Ruvuma.

"Sisi tunatumia muda huu ligi imesimama kufanya marekebisho madogo kwenye timu na pia tunafanya maandalizi kwa michezo yetu ijayo..., katika kipindi hiki tumepanga kucheza michezo miwili ya kirafiki ," alisema Ongala.

Alisema moja ya mchezo huo wa kirafiki wamepanga kucheza dhidi ya JKT Mlale ya Songea.

Alisema, wanajua mchezo wao unaofuata wanacheza na mabingwa watetezi, Yanga hivyo wanajiandaa kikamilifu kuhakikisha wanapata pointi kwenye mchezo huo.

"Tutacheza na Yanga ligi itakapoendelea, walitufunga mchezo wa kwanza, lakini kwa huu, tunajipanga kuhakikisha hatupotezi pointi," alisema Ongala.

Majimaji inashika nafasi ya 14 kati ya 16 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 17 baada ya kucheza michezo 18.

Habari Kubwa