Majonzi Yanga

21Nov 2016
Mahmoud Zubeiry
Dar es Salaam
Nipashe
Majonzi Yanga
  • ***Busungu apata ajali, mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo afariki dunia baada ya kuugua…

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Malimi Busungu juzi joni alipata ajali eneo la Dakawa, Morogoro akiwa njiani kuelekea Dodoma.

Hata hivyo, bahati nzuri mchezaji huyo hakuumia zaidi ya gari lake aina ya Subaru kuharibika vibaya eneo lote la mbele.

Meneja wa Busungu, Mohammed Yahya ‘Tostao’ aliliambia Nipashe jana kwamba, Busungu ndiye aliyekuwa chanzo cha ajali hiyo baada ya kuligonga gari lililokuwa mbele yake.

“Unajua tena vyombo vya moto hivi, inawezekana gari lake breki zilifeli, basi akaenda kulivaa gari la mwenzake kwa nyuma.

Gari la Busungu ndilo lililoumia zaidi, lakini tunashukuru yeye mwenyewe hajaumia, alikuwa analalamika kuumwa tumbo kidogo tu,”alisema Tostao.

Tostao alisema hiyo ni ajali ya pili mfululizo ndani ya miezi miwili, baada ya mwezi uliopita pia kupata ajali mbaya barabara hiyo, lakini akatoka salama.

Alisema kwa sasa gari zote mbili zinashikiliwa Kituo cha Polisi Dakawa kwa uchunguzi zaidi na Busungu amerejea kwao, Mzumbe mjini Morogoro.

Busungu hajaichezea Yanga tangu Oktoba, baada ya kususa kufuatia kukata tamaa kutokana na kutopewa nafasi ya kucheza chini ya kocha Mholanzi Hans van der Pluijm na alikuwa anashinikiza kuondoka.

Lakini katikati ya mwezi huu alisema kwamba amesitisha uamuzi wake wa kuondoka Yanga baada ya mabadiliko ya benchi la Ufundi yanayotaka kufanywa na uongozi, kwa kumpa mikoba ya Pluijm Mzambia George Lwandamina

MSIBA
Wakati huo huo, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Muda ya Yanga, Isaac Shekiondo ‘Clinton’ amefariki dunia usiku wa kuamkia jana.

Taarifa iliyotolewa na familia yake jana, ilieleza kuwa, marehemu alifariki dunia baada ya kuugua kwa muda na msiba upo nyumbani kwake, Ilala Mchikichini Kota.

Shekiondo alikuwa Makamu Mwenyekiti katika Kamati ya Muda ya Yanga chini ya Mwenyekiti, Tarimba Abbas ‘Thabo Mbeki’ na enzi zake anakumbukwa kutokana na ukarimu wake na uwajibikaji mzuri.

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi alisema amezipokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa Shekiondo.

“Kwa kweli nimezipokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa Shekiondo. Namfahamu vizuri yule bwana, tumefanya naye kazi Yanga. Na tulikuwa naye kwenye mpira siku zote,”alisema Malinzi.

Rais wa zamani wa Yanga, Francis Kifukwe naye pia alisema amezipokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa Shekiondo.
“Kwa kweli ni msiba wetu sote wana Yanga.

Shekiondo tulikuwa naye Yanga tena katika kipindi kigumu sana, lakini tulishirikiana vizuri kusukuma mbele gurudumu la timu.

Mungu amuweke pema peponi,”alisema Kifukwe. Bwana ametoa, bwana ametwaa. Mungu ampumzishe kwa amani marehemu Shekiondo.

Habari Kubwa