Makambo aomba uraia akipige Stars

26Aug 2018
Somoe Ng'itu
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Makambo aomba uraia akipige Stars

MSHAMBULIAJI nyota raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), anayeichezea Yanga, Heritier Makambo, anajiandaa kuomba uraia wa Tanzania, imefahamika.

MSHAMBULIAJI nyota raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), anayeichezea Yanga, Heritier Makambo.

Taarifa za kubadilisha uraia zinatokana na mshambuliaji huyo ambaye amekuwa kipenzi cha Yanga kutaka kutengeneza mazingira ya kuichezea timu ya Taifa ya Tanzania maarufu Taifa Stars.

Akizungumza na gazeti hili jana, mmoja wa viongozi wa juu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), alisema Makambo amefikia uamuzi huo baada ya kuona kuwa nafasi yake ya kuitwa katika kikosi cha Kongo ni finyu.

Kiongozi huyo alisema tayari shirikisho limeanza kufuatilia taratibu za kubadilisha uraia, lakini bado linasema mwenye uamuzi wa kumuita mshambuliaji huyo katika kikosi cha Taifa Stars ni Kocha Mpya Mnigeria, Emmanuel Amunike.

"Endapo Makambo atafanikiwa kubadilisha uraia hatakuwa mchezaji wa kwanza, na sisi tunahitaji kuwa na kikosi imara na kipana, tusubiri kwanza abadilishe uraia na kiwango chake kitakuwa vipi wakati huu wa vita ya kuelekea fainali za AFCON," alisema kiongozi huyo.

Makambo alifunga bao la kwanza wakati Yanga ikipata ushindi wa mabao 2-1 katika mechi yake ya raundi ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara pale walipoikaribisha Mtibwa Sugar kutoka Manungu, Morogoro.

Hata hivyo, Makambo alishindwa kuichezea timu yake katika mechi dhidi ya USM Alger ya Algeria kutokana na kukosa kibali cha uhamisho (ITC), ambayo wawakilishi hao pekee wa Tanzania waliobakia katika mashindano ya kimataifa walipata ushindi wa kwanza na kufikisha pointi nne.

Mshambuliaji huyo aliyesajiliwa na Kocha Mwinyi Zahera anatarajia pia kuongoza safu ya ushambuliaji katika mechi ya Kundi D ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rayon Sports itakayopigwa Agosti 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa Kigali, Rwanda.

Habari Kubwa