Makocha kibao waitaka Simba

28Jun 2018
Somoe Ng'itu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Makocha kibao waitaka Simba

HUKU Kamati ya Usajili ya Simba ikiendelea na mchakato wa kusajili wachezaji wapya, makocha kutoka nchi mbalimbali wameanza kuwasilisha maombi ya kurithi mikoba ya Mfaransa, Pierre Lechantre.

Mohammed 'Mo' Dewji.

Mfaransa huyo ambaye alipewa mkataba wa miezi sita, aliamua kuisusa timu hiyo ilipokuwa Kenya katika mashindano ya Kombe la SportPesa na baada ya siku chache aliondoka nchini na kurejea kwao.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa kwa kushirikiana na mwekezaji, Mohammed 'Mo' Dewji, bado hawajafikia uamuzi wa kocha yupi atue nchini kuungana na Masoud Djuma ili kuwanoa mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka pale uongozi mpya wa klabu hiyo utakapopatikana.

Chanzo hicho kiliendelea kusema kuwa mambo mengi ndani ya klabu hiyo yanashindwa kuamuliwa kutokana na mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo ambayo inasubiri kusajili upya.

"Simba ni klabu kubwa na sasa taarifa zake ziko kila mahali, kuondoka tu kwa Lenchatre kulifungua milango kwa makocha wengine kutuma maombi, ila kamati ya utendaji inachelea kufanya uamuzi mpya kwa sababu ya kutokuwa na nguvu, bado Masoud (Djuma) ataongoza jahazi," alisema mmoja wa viongozi wa juu wa klabu hiyo.

Habari Kubwa