Makocha Simba, Lipuli wafunguka

28Feb 2019
Somoe Ng'itu
Iringa
Nipashe
Makocha Simba, Lipuli wafunguka

WAKATI kikosi cha Simba kilianza safari ya kuelekea Shinyanga jana asubuhi kwa ajili ya kwenda kuwavaa wenyeji Stand United, Kocha Msaidizi wa Simba, Dennis Kitambi, ametoa sababu ya kushinda dhidi ya Lipuli FC juzi, huku akitamba kikosi chao kimejipanga kuzoa pointi tatu katika kila mchezo wa Ligi

Kitambi ambaye ametua kwa mabingwa hao watetezi akitokea AFC Leopards ya Kenya, alitoa kauli hiyo baada ya Simba kuichapa Lipuli FC mabao 3-1 katika mchezo wake wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa juzi mkoani hapa.

Akizungumza na gazeti hili, Kitambi alisema licha ya ratiba ngumu waliyokuwa nayo, wamejipanga vema kuhakikisha wanashinda mechi zao zote ili waweze kutetea ubingwa wa ligi hiyo wanaoushikilia.

Kitambi alisema pamoja na changamoto walizonazo, bado kikosi chao kimejipanga kupata matokeo mazuri na kutimiza malengo ambayo wameyaweka katika msimu huu.

"Walisema Simba imezoea kutoka sare na Lipuli, sasa tulipokuja hapa tulisema hapana, tunataka kumaliza hii rekodi na kupata ushindi, tunahitaji kuzoa pointi tatu katika kila mechi tutakayocheza kwenye ligi hii," alisema kocha huyo wa zamani wa Ndanda FC na Azam FC zote za Tanzania.

Alisema pia mbali na wachezaji kujituma, alitaja sababu nyingine iliyowapa ushindi katika mchezo huo ni kutoa nafasi kwa kila mchezaji wa timu hiyo kuonyesha uwezo wake jambo ambalo limekuwa likisaidia kutimiza malengo ya kupata ushindi.

Naye Kocha Mkuu wa Lipuli FC, Selemani Matola, ambaye timu yake ina pointi 38, aliliambia gazeti hili kuwa makosa yaliyofanywa na safu yake ya ulinzi ndio yamewagharimu katika mchezo huo ambao awali aliamini wataendelea kuisumbua Simba.

Hata hivyo, Matola alisema kuwa Simba iko katika kiwango kizuri na ilistahili kushinda kutokana na namna walivyojipanga.

"Simba ni timu bora, hakuna ambaye hajui ubora wa Simba kwa sasa, ni timu inayoundwa na wachezaji wenye uzoefu na wanaopata huduma zote muhimu, tumepoteza mchezo huu, hatujakata tamaa, tutajipanga upya kwa ajili ya mchezo ujao," alisema kocha huyo ambaye Jumapili iliyopita alitinga robo fainali ya Kombe la FA.

Aliongeza kuwa kikosi chake kilitarajia kuanza safari ya kuelekea Bukoba jana mchana kwa ajili ya kwenda kuwavaa wenyeji wao Kagera Sugar katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Habari Kubwa