Makocha, viongozi waipongeza Simba

30Jun 2020
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Makocha, viongozi waipongeza Simba

MAKOCHA na viongozi mbalimbali nchini na nje ya nchi, wameipongeza klabu ya Simba kwa kutwaa ubingwa wa soka Tanzania Bara kwa msimu wa 2019/20, ikiwa ni kwa mara ya tatu mfululizo.

Makocha na viongozi hao wamesema kuwa ubingwa wa Simba hautokani tu na kikosi kizuri walichonacho, lakini mipango, matunzo na uwekezaji wa klabu hiyo.

Kocha wa Prisons, Mohamed Rishard Adolf, ameipongeza Simba na kusema kuwa ilikuwa na kikosi kizuri, chenye wachezaji wazuri waliokamilika kila idara, lakini uongozi wao pamoja na uwekezaji ambao umefanyika ndani ya klabu hiyo ndiyo unaowafanya kuwa na ubora huo.

"Tunashukuru kwa sare tulioipata, tulitaka pointi tatu, lakini tumepata moja, tumebakisha mechi sita, tunajua huko mbele nini tutafanya," alisema kocha huyo baada ya kikosi chake kutoka sare ya bila kufungana kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars, Bakari Shime naye pia ameipongeza klabu ya Simba na kusema kuwa timu hiyo ilistahili kuwa mabingwa kutokana na kuonekana kama vile haikuwa na upinzani wa kutosha kutoka kwa timu zingine.

Msemaji wa Yanga, Hassan Bumbili alisema kuwa anawapongeza Simba, lakini wao kama Yanga wanachofanya kwa sasa ni kutengeneza kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao na hawana uhakika wanachukua kama ligi ikiendeshwa kwa haki.

Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, aliwapongeza wapinzani wake kwa kutwaa ubingwa huo.

Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), nayo pia kwenye ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii, liliwapongeza mabingwa wao mara tatu mfululizo kwa kutwaa ubingwa wa Tanzania.

Baada ya sare ya bila kufungana dhidi ya Prisons, Simba imefikisha pointi 79 ambazo haziwezi kufikishwa na timu nyingine yoyote ile Ligi Kuu.

Habari Kubwa