Makonda, Spika wafunguka Simba inavyopaisha uchumi

19Mar 2019
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Makonda, Spika wafunguka Simba inavyopaisha uchumi

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Spika wa Bunge, Job Ndugai, kwa nyakati tofauti wameipongea Simba kwa kufanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku wakieleza kuwa mafanikio hayo licha ya kuitangaza Tanzania kimataifa, yataliongezea taifa ....

Mwenyekiti wa Kamati ya Ushindi ya Taifa Stars, Paul Makonda (wa pili kulia), akizungumza jijini Dar es Salaam jana kuhamasisha mashabiki wa soka kujitokeza kwa wingi Jumapili kuishangilia Stars itakapokuwa ikicheza na Uganda. Wengine ni wajumbe wa kamati hiyo, Mhandisi Hersi Said (kulia), Philimon Ntalihaja (kushoto) na Athumani Nyamlani. PICHA: Somoe Ng'itu

pato la kiuchumi pindi wapinzani wa timu hiyo watakapokuja kucheza dhidi yao hapa nchini.

Simba iliyokuwa katika Kundi D imesonga mbele katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuifunga AS Vita kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kufikisha pointi tisa, huku kinara wa kundi hilo, Al Ahly ikimaliza na pointi 10.

Akizungumza jana jijini, Makonda alisema kuwa wafanyabiashara mbalimbali wakiwamo wenye hoteli, usafiri na chakula hufanya biashara kwa kuwahudumia wagezi (timu) wanaokuja nchini kwa ajili ya kucheza na Simba na hivyo pato la uchumi huongezeka.

Makonda alisema mafanikio yaliyofikiwa na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara watalifanya jina la Tanzania kuendelea kutajwa katika medani za kimataifa na wachezaji watapata nafasi ya kunadi vipaji vyao.

Pia aliwapongeza mashabiki wa Simba kwa kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yao na kusema kwamba walitimiza jukumu lao la kuwa mchezaji wa 12 uwanjani.

"Hongera sana Simba, hongera wote walioshiriki kufanikisha ushindi ule, huu ni ujumbe mkubwa kwa serikali na Afrika kuwa mpira ni jadi yetu na tuna mahaba makubwa, " alisema kiongozi huyo.

Aliongeza kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli kwa kuwekeza katika michezo na kuamua kujenga uwanja mwingine wa michezo wa kisasa ambao utakuwa na uwezo wa kuingiza mashabiki zaidi ya 100,000.

"Sasa Simba wameonyesha Tanzania sio Shamba la Bibi...wametupa matumaini mapya, tutajisikia hafari kupata uwanja huo mpya, ametupa deni," Makonda alisema.

Kwa upande wake Spika Ndugai mbali na kuipongeza Simba, wakati akizindua Ofisi ya Shirika la Ndege nchini(ATCL) jijini Dodoma jana, alisema kwa sasa nchi ya Congo na Misri wanaifahamu Tanzania na hivyo michezo hiyo itakuwa imetangaza ndege za ATCL.

“Tunapoendelea kuitangaza nchi yetu nitumie nafasi hii pia kuipongeza Klabu ya Simba kwa walichokifanya Jumamosi kwa kuifunga AS Vita, wapo watakaonuna, lakini nasema kwa dhati DRC Kongo nchi kubwa hakuna asiyejua neno Tanzania kupitia mpira ule,”alisema.

Alisema kwa mtu mpenda michezo hakuna ambaye atakuwa hajui nchi inayoitwa Tanzania kwa sababu imetangazwa sana na ATCL itakapotaka kuelekea eneo hilo ina faida za ziada kupata wateja.

“Vivyo hivyo mpenda mpira wa Misri, Al Ahly ambayo ni klabu namba moja kule imepigwa, inaijua Tanzania, Algeria hivyo hivyo, kwa hiyo kwa kupitia michezo imetangaza nchi kwa kiwango ambacho huwezi kuamini,” alisema.

Imeandaliwa na Somoe Ng'itu, Dar na Augusta Njoji, DODOMA

Habari Kubwa