Makonda, wanamichezo Temeke kuteta

21Mar 2016
Nipashe
Makonda, wanamichezo Temeke kuteta

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda anatarajia kukutana na klabu za jogging, wasanii na wanamichezo mbalimbali Aprili 7 mwaka huu kwa ajili ya kujadili kuinua viwango vya michezo jijini.

PAUL MAKONDA

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda anatarajia kukutana na klabu za jogging, wasanii na wanamichezo mbalimbali Aprili 7 mwaka huu kwa ajili ya kujadili kuinua viwango vya michezo jijini.

Makonda alitoa ahadi ya kukutana na wanamichezo hao baada ya kumaliza mazoezi ya jogging yaliyofanyika jana chini ya Chama cha Jogging Temeke (TEJA) kwa kushirikiana na msanii wa muziki wa asili, Mrisho Mpoto.

Alisema amefurahi kuona vijana na wazee wanajitokeza kuunda klabu hizo na kusaidia kujenga afya ya miili yao.
Alisema mazoezi yanayofanywa na klabu hizo ni moja ya changamoto ya kuwavuta vijana kujiunga katika michezo na kuacha dhana potofu ya kubweteka na kufikiria kufanya vitendo viovu.

"Nafurahi hiki mlichokifanya TEJA na Mpoto huu ni mwanzo, muendelee na umoja huo kuhakikisha mnazivuta klabu zote, "alisema Makonda.

Alieleza kuwa endapo wananchi wataendelea kukutana na kuendelea na mazoezi, kwake itakuwa rahisi kuomba fedha kwa Rais, John Pombe Magufuli ili kuwaendeleza vijana katika michezo na ujasiriamali.

Aliongeza kuwa katika mkutano huo wa Aprili 7, ametenga Sh. milioni 2 kwa ajili ya kuipa klabu ambayo itakuwa imekamilisha usajili wake na inayojiendesha chini ya uangalizi na viongozi waliochaguliwa kihalali.

Mpoto alisema ameamua kuungana na TEJA ili kuhakikisha Temeke na wanamichezo wake inafanikiwa kujitangaza kupitia vipaji vyao.

Habari Kubwa