Malinzi aonya kuchafuana uchaguzi TFF

16Apr 2017
Somoe Ng'itu
Nipashe Jumapili
Malinzi aonya kuchafuana uchaguzi TFF

KUELEKEA uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Rais wa shirikisho hilo, Jamal Malinzi, amewataka wadau wenye nia ya kuwania nafasi mbalimbali kwenye kinyang'anyiro hicho kutotumia lugha "chafu" dhidi ya wenzao kwa faida ya soka la nchini.

Jamal Malinzi

Uchaguzi wa TFF unatarajiwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu mahali ambapo patatangazwa hapo baadaye.

Akizungumza na gazeti hili muda mfupi baada ya kurejea nchini kutoka Morocco alipoenda kuwasalimia wachezaji wa Serengeti Boys, Malinzi alisema kujiepusha na maneno ya kuchafuana kutasaidia kuendelea kuvutia wadhamini ambao bado wanahitajika kwenye soka la Tanzania.

Malinzi alisema ligi na mashindano yanayofanyika hapa nchini yanategemea wadhamini na amewataka wagombea kujipanga kuwania madaraka na si kufanya vitendo vitakavyoichafua TFF.

"Imetumika nguvu kubwa kuijenga taasisi tangu ilipokuwa FAT (Chama cha Soka Tanzania) mpaka leo hii inaitwa TFF, kikubwa tuache malumbano, vurugu zozote zitachangia kukimbiza wadhamini kwenye mpira wetu," alisema Malinzi ambaye aliwahi pia kuwa Katibu Mkuu wa Yanga.

Aliongeza kuwa wagombea wawe na subira muda utakapofika watatakiwa kufuata taratibu zitakazotangazwa kwa mujibu wa katiba.

Katika uchaguzi huo, nafasi zitakazowaniwa ni ya Urais, Makamu wa Rais na wajumbe wa Kamati ya Utendaji kutoka katika Kanda 13.

Malinzi alishinda nafasi ya urais baada ya kumwangusha aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF, Athumani Nyamlani.