Manara 'ajilipua' Simba kwa Yanga

10Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Manara 'ajilipua' Simba kwa Yanga

LICHA ya kuhudumu kwa mabingwa wa nchi, Simba kwa kipindi kirefu akiwa Ofisa Habari wa klabu hiyo, Haji Manara, amesema yeye hajawahi kuwa na mapenzi na timu hiyo, huku akitaka kwa sasa aulizwe mambo yanayohusu klabu yake ya Yanga pekee, anakofurahia maisha zaidi ya alikotoka.

Akizungumza na mwandishi wetu Dar es Salaam jana, Manara ambaye kwa sasa amehamia upande wa pili kuwa msemaji wa klabu hiyo, alisema katika maisha yake hajawahi kuwa Simba na kwamba yeye ni Yanga na kama kuna ukubwa aliwahi kuwaaminisha Wanasimba, basi huenda alikuwa amelewa.

"Moja ya kazi kubwa niliyoifanya labda ni kuonyesha ukubwa 'feki', hiyo dhambi niliitenda vibaya sana kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nipo tayari kuhukumiwa hata [kwenda] gerezani kwa kufanya ulaghai wa 'kufiksi' ukubwa ambao haupo," alisema.

Aliongeza kuwa Yanga ndiyo klabu kubwa na yenye mataji mengi zaidi vinginevyo ni uongo ambao yeye mwenyewe hapo nyuma alishiriki kuupika.

Alisema watu ambao wapo maalumu kwa ajili ya kumchafua, atawashughulikia vizuri kwa kuwa anajua kila kitu kinachoendelea.

Wakati Manara akisema hivyo, takwimu zinaonyesha kwa ujumla Simba ndiyo klabu iliyobeba makombe mengi (mara 51) yanayojulika nchini wakati Yanga inayoongoza kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu (mara 27 dhidi ya watani zao walioubeba mara 22), yenyewe kwa mataji yote kwa ujumla ikifanya ikibeba mara 48 pekee.