Manispaa yatengua mtaa wa Wanyama

26Jun 2017
Faustine Feliciane
Nipashe
Manispaa yatengua mtaa wa Wanyama

SIKU moja baada ya kutangazwa kuupa jina la kiungo nyota wa Tottenham na timu ya Taifa ya Kenya, Victor Wanyama, mtaa wa Viwandani Shekilango, Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo imetengua uamuzi huo.

Taarifa ya Manispaa hiyo imesema kwamba imechukua hatua hiyo kwa sababu jambo hilo lilifanyika kinyume cha utaratibu.

“Majina ya mitaa hupendekezwa na kamati za mitaa husika kisha hupelekwa kwenye vikao vya WDC vya kata halafu uamuzi wa WDC hupelekwa kwa mkurugenzi kwa ajili ya kuingizwa kwenye kikao cha Kamati ya Fedha na uongozi, Baraza la Madiwani.

"Mwisho suala hilo linapelekwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa ajili ya kuidhinishwa, lakini kwa Wanyama utaratibu huo haujafuatwa," ilisema taarifa ya manispaa hiyo.

Suala la hodha huyo kupewa heshima ya mtaa huo jina lake, lilizua gumzo kwenye mitandao ya kijamii huku wengine wakitaka nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, kupewa heshima kama hiyo.

Wanyama alikuwa nchini kwa mapumziko baada ya kumalizika Ligi Kuu ya England.

Habari Kubwa