Manuel Pellegrini Ndoto 'yapeperuka' Ulaya


06May 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Manuel Pellegrini Ndoto 'yapeperuka' UlayaKOCHA wa Manchester City, anamaliza misimu mitatu ya kufundisha Uwanja wa Etihad, England bila kutwaa taji baada ya kikosi chake kufungwa bao 1-0 na Real Madrid ya Hispania katika mechi ya marudiano Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyochezwa juzi usiku kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu.


Matokeo hayo yana maana, fainali ya mwaka huu Ligi ya Mabingwa Ulaya inazikutanisha Real Madrid na Atletico Madrid - timu kutoka mji moja na nchi moja.
Ni kama fainali ya marudiano na kisasa, kwani timu hizo mbili za Hispania ziliwahi kukutana mwaka 2014 na Real kushinda 4-1 baada ya kucheza dakika 120.
Fainali hiyo itapigwa Mei 28 kwenye Uwanja wa San Siro, mjini Milan Italia.


Ni fainali ya tatu katika miaka minne timu kutoka taifa moja zinakutana.
Hii ni mara ya tatu kwa Manchester City kutolewa na timu za Hispania kwenye michuano hiyo, Real Madrid wakifanya hivyo mara mbili na mara moja Barcelona.


Pellegrini alikuwa na ndoto ya kuondoka Etihad japo akiwa na taji la Ulaya baada ya kukosa ubingwa wa England uliotua mikononi mwa Leicester City.
Katika mchezo wa kwanza zaidi ya wiki moja iliyopita timu hizo zilishindwa kufungana, hivyo kuipa nafasi ndogo City kusonga mbele dhidi ya miamba hiyo ya soka Hispania na mabingwa wa mara tisa Ulaya.


Pellegrini anaondoka mwishoni mwa msimu huu kumpisha Pep Guardiola, ambaye naye misimu yake mitatu akiwa Bayern Munich ameshindwa kuipa taji la ubingwa Ulaya.
Pamoja na kushinda mabao 2-1 dhidi ya Atletico Madrid ya Hispania katika mechi ya marudiano - nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Bayern waliaga kwa faida ya bao la ugenini la vijana wa kocha Diego Simeone.


Hata hivyo, Pellegrini - raia wa Chile, anaondoka City akiweka rekodi ya pekee na aina yake, kwani ndiye kocha wa kwanza kuiwezesha timu hiyo kucheza nusu fainali Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya kwanza.
Kwa Real Madrid, kusonga kwao mbele na kucheza hatua ya nusu fainali ni mwendelezo wa rekodi nzuri.


Mabingwa hao wa mara tisa Ulaya, wanacheza fainali Ulaya kwa mara ya 14, rekodi ambayo haijafikiwa na timu zingine.
Miamba hiyo ya Hispania haijapoteza mechi zote sita ilizocheza kwenye uwanja wa nyumbani Ligi ya Mabingwa msimu, huku mshambuliaji wake, Cristiano Ronaldo akicheza nusu fainali ya 17 tangu alipotua Bernabeu, akifikisha idadi sawa ya michezo na Xabi Alonso.
Katika mechi hiyo, shujaa wa mchezo aliyeivusha Madrid alikuwa Gareth Bale

aliyeukwamisha wavuni mpira kwa shuti la pembeni lilikomgusu Fernando na kumshinda kipa Joe Hart.
Katika mechi hiyo, Madrid walitawala kwa tofauti ya asilimia 15 dhidi ya Man City walioweza kufumua mashuti matano na moja tu likilenga lango, huku wenyeji wao wakifyatua michomo 15 na mitano ikilenga lango alilosimama kipa Hart.

Habari Kubwa