Manula aiota tuzo ya Afrika

21Jul 2021
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Manula aiota tuzo ya Afrika

GOLIKIPA chaguo la kwanza la mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Aishi Manula amesema ameshafanya kila kitu kwenye soka la hapa nchini na sasa akili yake anaielekeza kuwania tuzo ya mlinda mlango bora wa Afrika.

Manula ambaye alitua Simba akitokea Azam FC mwaka 2017, pia ndiye golikipa namba moja wa Timu ya Soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars).

Nyota huyo alisema hayo wakati akizungumzia mafanikio yake baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2020/21 iliyomalizika Jumapili iliyopita, ambapo huu ni msimu wa sita mfululizo anashinda tuzo hiyo baada ya kuongoza kwa kutoruhusu mabao kwenye mechi nyingi kuliko makipa wengine.

"Huu ni msimu wa sita mfululizo sasa naongoza kwa 'clean sheet', na kuwa kipa bora. Nimeshazoea sasa na hata shabiki yoyote au wanahabari wakisikia Manula kipa bora hakuna anayeshtuka kwa sasa. Kila mtu anaona kawaida. Hata mimi mwenyewe naona kawaida, " alisema Manula.

Alisema lengo lake kwa sasa ni kushindana na magolikipa wakubwa katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa na kutwaa tuzo ya kipa bora wa Afrika.

"Sasa nataka niende juu kidogo kwa sababu huku chini nimeshamaliza, ninataka nishindane nipate 'clean sheet' za kutosha kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, ili nichukue tuzo huko," alisema golikipa huyo.

Manula amemaliza Ligi Kuu Tanzania Bara 2020/21 akiwa na 'clean sheet' 18, akifuatiwa na kipa wa Mbeya City, Haroun Mandanda ambaye amesimama golini mara 15 bila kuruhusu wavu wake kutikiswa huku Metacha Mnata wa Yanga na Abutwalib Mshery wa Mtibwa Sugar, wana 'clean sheet' 13 kila mmoja.

Kipa mkongwe, Juma Kaseja, yeye amesimama langoni mara 11 bila kuruhusu bao pamoja na Aaron Kalambo wa Dodoma Jiji, huku Daniel Mgore wa Biashara United akiwa na 'clean sheet' 10.