Maproo wainyima usingizi Azam FC

23May 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Maproo wainyima usingizi Azam FC

WAKATI kipenga cha kurejea kwa Ligi Kuu Tanzania Bara kimeshawaka, mabosi wa Azam FC 'wanaumia kichwa' kwa sababu ya kuwakosa wachezaji wake wa kimataifa saba ambao bado hawajarejea nchini, imeelezwa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin:PICHA NA MTANDAO

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat' aliliambia gazeti hili kukosekana kwa wachezaji hao wa kimataifa kutakuwa ni pengo kwa kikosi chao.

Popat alisema licha ya Tanzania kufungua anga yake, lakini nchi nyingine zikiwamo Ghana, Zimbabwe na Uganda bado hawajafungua mipaka na viwanja vyao vya ndege.

"Tumepata taarifa Ghana wanatarajia kufungua mipaka yao Juni 15, mwaka huu na huko kuna wachezaji wetu watatu (Razak Abalora, Yakub Mohammed na Daniel Amoah)," alisema Popat.

Aliwataja wachezaji wao wengine ambao hawako nchini ni pamoja na Mganda Nicholas Wadada, Never Tigere, Donald Ngoma na Bruce Kangwa walioko Zimbabwe.

"Leo (jana) Bodi ya Ligi na Wizara zilitarajia kukutana, tunasubiri taarifa kutoka kwao ikiwa ni kuanza rasmi Juni Mosi, kwetu itakuwa ni changamoto, sasa vichwa vinauma juu ya kuwakosa wachezaji wetu hawa lakini pia na makocha," alisema Popat.

Alisema Kocha Mkuu Arastica Cioaba alirejea kwao Romania huku msaidizi wake, Vivier Bahati ambaye ni raia wa Burundi pia alikwenda kwao.

"Inapofika kwa makocha hapo ni mtihani, maana walimu wetu wote kutoka nje, wawili kutoka Romania na mmoja Mrundi, yeye hapa Burundi tuna imani hakuna shida," Popat alisema.

Alimtaja mshambuliaji pekee aliyebakia ambaye ataongoza safu ya ushambuliaji ni Mzambia Obrey Chirwa.

Habari Kubwa