Mapya Yanga kukodishwa

10Aug 2016
Na Mwandishi Wetu
Lete Raha
Mapya Yanga kukodishwa

MJUMBE wa Baraza la Wadhamini la Yanga, Francis Kifukwe, amemtaka mfanyabiashara anayetaka kuikodisha klabu hiyo kuwasilisha mapendekezo yake kwa maandishi.

Akizungumza na Lete Raha jana jijini Dar es Salaam, Kifukwe alisema baada ya mkutano wa Jumamosi, alimwambia mfanyabiashara anayetaka kuikodisha timu kwa miaka 10, awasilishe maombi yake kwa maandishi.

“Tunasubiri mapendekezo yake rasmi katika maandishi, ili sisi (Baraza la Wadhamini) tuanze kuyafanyia kazi,”alisema Kifukwe jana.

Hiyo inamaanisha pamoja na wanachama wa Yanga kukubali kubadilisha mfumo wa kuiendesha klabu na kuafiki kuimilikisha kwa mtu mmoja, lakini watalazimika kusubiri taratibu zifuatwe.

Katika mkutano mkuu wa dharura uliofanyika Jumamosi ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, wanachama wa Yanga walikubali kuikodisha kwa mtu klabu yao kwa miaka 10 baada ya mwanachama mmoja kutoa pendekezo la kuikodisha ikiwa ni pamoja na kumilikishwa nembo na timu na katika kipindi hicho, atakuwa anachukua asilimia 75 ya mapato ya timu, huku asilimia 25 ikibaki kwa wanachama.

Hata hivyo, katika mkutanuo huo, wanachama watatu wa klabu hiyo, Ayoub Nyenzi, Salum Mkemi na Hashim Abdallah walifukuzwa, wakati mmoja, Siza Lyimo alinusurika baada ya kuomba msamaha na kusamehewa.

Habari Kubwa