Mashabiki wa Madrid, Barca wazawadiwa Dar

26Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mashabiki wa Madrid, Barca wazawadiwa Dar

USHINDI wa mabao 3-1 wa Real Madrid dhidi ya mahasimu wao, Barcelona umenogeshwa na chemsha bongo ya Kampuni ya Michezo ya Kubahatisha ya M-Bet Tanzania na mashabiki wa soka kujishindia zawadi mbalimbali.

Tukio hilo lilifanyika kwenye Baa ya Tips Mikocheni ambapo mbalimbali ya mashabiki kuzawadiwa zawadi mbalimbali zikiwamo jezi halisi 'orijino' za timu hizo mbili, pia walipata fursa ya kupiga picha na mfano wa Kombe LaLiga ambalo Real Madrid ilishinda msimu uliopita.

Mabao ya Real Madrid katika mechi hiyo ya juzi, yalifungwa na Federico Valverde, Sergio Ramos (kwa njia ya penati) na Luka Modric wakati lile la kufutia machozi la Barcelona lilifungwa na Ansu Fati.

Meneja Masoko wa Kampuni ya M-Bet Tanzania, Allen Mushi, alisema wameamua kuwachangamsha mashabiki wa soka Ligi ya Hispania kutokana na ushirikiano wao na La Liga.

Mushi alisema wamefikia uamuzi wa kuwazawadia mashabiki wa soka kama kutambua mchango wao katika shughuli zao za michezo ya kubahatisha.

Alisema maswali yao mengi yamelenga ufahamu kuhusiana na LaLiga kama mchezaji gani aliyefunga mabao mengi, wachezaji maarufu waliocheza ligi hiyo, mchango wa Cristiano Ronaldo na Lionel Messi katika timu zao, umaarufu wao na makocha.

“M-Bet imeingia mkataba na LaLiga katika kuendeleza soka la vijana ili kuleta maendeleo ya soka kwa timu zetu na timu ya Taifa, kabla ya kuanza kuendesha mafunzo mbalimbali, tumeamua kuanza kutoa zawadi kwa mashabiki

Mbali ya mechi ya Clasico, tutaendelea kutoa zawadi katika mechi nyingine mbalimbali za Ligi ya Hispania na kutoa elimu ya ufahamu wa ligi hiyo kwa mashabiki wa soka,” alisema.

Habari Kubwa