Mashabiki wa Simba na Yanga roho juu

17Feb 2016
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Mashabiki wa Simba na Yanga roho juu

BADO siku tatu Simba na Yanga zishuke dimbani Taifa, lakini nyuma yake mashabiki wa timu hizo roho zao ziko juu-juu kuelekea mtanange huo.

SIMBA

Hii siyo mara ya kwanza kwa mashabiki wa timu hizo kuwa roho juu, lakini hapana shaka safari hii kurukaruka kwa roho ni kukubwa zaidi.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, mashabiki hao walisema mchezo huo wa watani huwa na matokeo ya kushangaza na wakati mwingine huweka pembeni ubora wa timu hizo.

Abdallah Mussa, mwanachama wa Simba mwenye kadi namba 774 alisema jana kuwa licha ya kutokuwa na hofu na kikosi chao, lakini lolote linaweza kutokea.

"Tukiwakosa ni mapenzi ya Mungu, ila kasi ya Simba iko juu, wachezaji wana ari na morari, pia wanajiamini kutokana na matokeo ya mechi zao za ligi zilizopita, hakuna kuhofia, tuje kwa wingi uwanjani," alisema Abdallah.

Peter Kadutu, shabiki wa Simba wa Kundi ya Simba Makini alisema anaamini Jumamosi wataibuka na ushindi, lakini amewataka wachezaji wake kuongeza umakini.

Mwanachama wa Klabu ya Yanga, Sudi Tall (1954) alisema kuwa wana kikosi kizuri hata hivyo, soka ni dakika 90.

"Wana-Yanga ninawaambia tuongeze dua, umoja na mshikamano, Simba wana timu nzuri, lakini Yanga tuna kikosi kizuri zaidi. Tulifanya usajili mzuri na tuna mwalimu makini, ila mpira ni dakika 90," alisema mwanachama huyo maarufu wa klabu hiyo ya Mtaa wa Jangwani na Twiga jijini.

Naye Carlos Andrew wa Yanga alisema wanaimini timu yao lakini inapofika suala la kukutana Simba, wanamuomba Mungu kwa sababu mechi hiyo hitabiriki.

Simba itashuka kuikabili Yanga huku wakiwa wanaongoza ligi hiyo baada ya kufikisha pointi 45, wakati mahasimu wao wana pointi 43 lakini wana mchezo mmoja pungufu.