Mashabiki wa Simba, Yanga waendelea kuchangia damu

11Jul 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Mashabiki wa Simba, Yanga waendelea kuchangia damu

KUELEKEA mechi ya hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Kombe la FA, kati ya Simba na Yanga itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam, chupa 200 za damu zinatarajiwa kuchangwa kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa waliolazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI).

Wadhamini wa klabu hizo mbili, Kampuni ya GSM kwa upande wa Yanga na Romario Sports, wanaoidhamini Simba, kwa pamoja wametoa jezi 200 kwa lengo la kuwapatia mashabiki wa timu hizo mbili ambao watajitokeza kuchangia damu katika taasisi hiyo.

Mhamasishaji wa mchakato huo, Azim Dewji, alitangaza mpango huo jijini jana, wakati wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu malengo na mikakati yake ya kusaidia kuokoa maisha ya Watanzania kupitia mechi za watani hao wa jadi.

Dewji alisema amekuwa akiguswa na changamoto ya upatikanaji wa damu kwa wagonjwa nchini, hivyo aliamua kuwashirikisha wadhamini wa timu hizo ambao walikubali kushiriki kwenye zoezi hilo litakalofanyika kuanzia leo.

“Tuliomba jezi 100 kwa Simba na 100 kwa Yanga, wote walitoa jezi hizo zenye thamani ya Sh. 15,000 kila moja, ambazo zitaanza kugaiwa kwa mashabiki wa timu hizo watakaojitokeza kuchangia damu kuanzia kesho (leo) hapa MOI,” alisema Dewji.

Aliongeza malengo yake ni kuchangia chupa 1,000 za damu kwa kila mwezi na baadaye wataendelea na zoezi hilo katika mikoa mingine hapa nchini.

Pia aliwahamasisha mashabiki wa timu hizo kuvaa barakoa watakaposhiriki katika mtanange huo kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa corona.

Naye Mkurugenzi wa Uzalishaji wa GSM, Hersi Said, alisema wapo tayari kuendelea kudhamini mpango huo kwa ajili ya kuchangia wagonjwa wanaohitaji damu.

“Tulipopewa taarifa na Mzee Dewji hatukuchukua dakika 10 kukubali, tunaahidi pia kuendelea kutoa zaidi kwa ajili ya kusaidia wagonjwa wanaohitaji damu ikiwezekana kufika mikoani,” alisema Said.

Mwakilishi wa Romario Sports, Mussa Mwambajingu, aliwataka mashabiki wa timu zote mbili kujitokeza kuchangia damu na kupata jezi za klabu hizo wanazozishabikia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tiba MOI, Dk. Samweli Swai, mbali na  kushukuru, alisema taasisi hiyo inahitaji chupa 30 hadi 40 kwa siku na chupa 900 hadi 1,000 kwa mwezi.

Aliwataja wahitaji wakubwa wa damu katika taasisi hiyo ni majeruhi wa ajali ambao wanalazimika kufanyiwa upasuaji wa mifupa mikubwa ya paja na upasuaji wa ubongo.

 

Habari Kubwa