Mashabiki waizuia Yanga Tunduma

16Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mashabiki waizuia Yanga Tunduma

KIKOSI cha Yanga kiliwasili jana mkoani Ruvuma kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Majimaji huku kikipokelewa kwa mbwembwe na mashabiki wa timu hiyo wilayani Tunduru.

Msafara wa timu hiyo ambao wametumia basi lao kusafiri, ulikutana na umati wa mashabiki wilayani Tunduru ambao walikuwa na shauku ya kutaka kuwaona wachezaji wa timu hiyo.

Mashabiki hao walizuia basi hilo la Yanga wakitaka kuwaona wachezaji wa timu hiyo.

Akizungumza na Nipashe jana, Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh, alisema, wamewasili mkoani humo salama na wachezaji wameelekeza akili zao kwenye ushindi.

"Tunashukuru tumefika salama, na sote mawazo yetu tumeyaelekeza kwenye mchezo dhidi ya Majimaji, wachezaji wapo katika hali nzuri ," alisema Saleh.

Aidha, alisema kocha wa timu hiyo, George Lwandamina, aliongea na wachezaji wake muda mfupi kabla hawajaanza safari ya kuelekea mkoani humo.

"Kocha anataka ushindi kwenye mchezo huu, hilo ameliweka wazi, na wachezaji wanafahamu umuhimu wa ushindi kwenye mchezo huu, kwa sababu ligi imekuwa na upinzani mkubwa," alisema Saleh.

Yanga inashuka kwenye Uwanja wa Majimaji kesho Jumanne kuumana na wenyeji wao Majimaji katika mchezo wa Ligi kuu Tanzania Bara.

Mchezo huo ni wa kwanza kwa Yanga tangu kumalizika kwa michuano ya Kombe la Mapinduzi Januari 13, mwaka huu.

Michuano hiyo ilisababisha Ligi kuu kusimama kwa majuma mawili kupisha ushiriki wa klabu za Simba, Azam na Yanga.

Habari Kubwa