Mashabiki Yanga, Simba waitwa Stars

19Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mashabiki Yanga, Simba waitwa Stars

MASHABIKI wa Simba, Yanga na klabu nyingine za soka hapa nchini wametakiwa kujitokeza kuishangilia Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars) katika mechi ya kufuzu Fainali za Afrika itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jana jijini, Mwenyekiti wa Kamati ya Ushindi ya Taifa Stars, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema umefika wakati kwa mashabiki wote kuungana na kuishabiki timu hiyo ili iweze kukata tiketi ya kushiriki fainali hizo.

Makonda alisema kuwa shabiki ni kiungo muhimu sana na anawaomba Watanzania wote kusimama na Taifa Stars kwa wakati huu.

"Ninawaomba watu wote tujitokeze kuiunga mkono Taifa Stars, tusimame na Stars, tuhakikishe tunaacha tofauti zetu, tuhakikishe kila mmoja anatimiza jukumu lake, tutumie fursa hii kuhakikisha Stars inashinda," alisema Makonda.

Alisema anahitaji kuona makundi yote yanajitokeza kuishangilia Taifa Stars na angetamani kuona Uwanja wa Taifa unajaa mara tatu ya walivyojitokeza mashabiki wa Simba katika mchezo wao dhidi ya AS Vita uliochezwa Jumamosi iliyopita.

"Sisi tunaunganishwa na Taifa Stars, tuitumie Stars kama sehemu ya kutuunganisha, AFCON 2019 ni zamu yetu," Makonda alisisitiza.

Habari Kubwa