Mastraika Yanga wamvuruga Kaze

23Feb 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Mastraika Yanga wamvuruga Kaze

LICHA ya timu yake kuendelea kushikilia rekodi ya kutopoteza mechi katika za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2020/21 unaoendelea, Kocha Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze, amesema bado ana kazi ya ziada ya kuimarisha safu yake ya ushambuliaji.

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Kaze alisema anaendelea kufanyia kazi upungufu uliyomo katika safu hiyo kwa kuongeza utulivu na umakini wa kutumia vyema nafasi wanazozitengeneza za kufunga mabao.

Kaze alisema pia anahitaji kuona washambuliaji wake wanakuwa watulivu wanapokuwa jirani na lango la mpinzani ili kujihakikishia ushindi mnono na mapema.

Mrundi huyo alisema wanahitaji kupata pointi tatu katika kila mechi ili kufikia malengo ambayo wanayatarajia na hatimaye kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na la mashindano ya Kombe ka FA.

“Hatuwezi kupata ushindi bila kufunga, tunatakiwa kuwa makini hasa katika nafasi tunazotengeneza kuhakikisha tunafunga mabao ili kuendelea kujiimarisha zaidi, kuendelea kubaki hapa juu tulipo, tunatakiwa kupambana na kila timu bila kujali nafasi na jina la mpinzani ambaye tunakutana naye,” alisema Kaze.

"Tunahitaji kupambana kupata matokeo mazuri katika mechi zilizopo mbele yetu, sasa tunaenda kujiandaa kwa ajili ya mchezo wa FA dhidi ya Kengold, hakuna mechi rahisi na kwa sababu tunacheza mfumo wa mtoano, hatutawadharau," alisema Kaze.

Yanga itaikaribisha Kengold katika mechi ya mzunguko wa nne wa Kombe la FA itakayochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini.

Habari Kubwa