Matola afunguka Simba ilivyokamiwa msimu huu

10Jul 2020
Somoe Ng'itu
Ruangwa
Nipashe
Matola afunguka Simba ilivyokamiwa msimu huu

KOCHA Msaidizi wa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Selemani Matola, amesema timu yao haikuwa na kazi rahisi katika safari yao ya kutetea ubingwa wa ligi hiyo inayotarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi huu.

KOCHA Msaidizi wa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Selemani Matola:PICHA NA MTANDAO

Simba ilifanikiwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa tatu mfululizo tangu Juni 28, mwaka huu, ilipotoka sare ya bila kufungana na Maafande wa Tanzania Prisons jijini, Mbeya.

Akizungumza na gazeti hili jana, Matola alisema mechi zote walizocheza msimu huu zilikuwa ngumu kwa sababu walikuwa wanapambana na klabu zinazoutamani ubingwa walioushikilia.

Matola alisema kila timu iliamini ikiwafunga Simba, itakuwa tumejiweka katika nafasi nzuri ya kuwania taji hilo na hivyo mechi zao zote zilikuwa na ushindani wa kiwango cha juu.

Nahodha huyo wa zamani wa Simba, alisema anawapongeza wachezaji wao kwa kupambana katika kila mechi waliyocheza na kutokana tamaa hata pale walipopoteza mchezo au walipolazimishwa sare.

"Safari yetu ilikuwa ngumu sana, ilikuwa tunapambana na timu zote 19, kila timu ilijipanga zaidi kutufunga ili kujiimarisha katika kutimiza malengo yake, kwa hiyo kila mchezo kwetu ilikuwa ni sawa na fainali, walijua wanacheza na bingwa mtetezi, watufunge ili wajirahisishie mipango yao," alisema Matola.

Aliongeza kuwa pongezi nyingine ziende kwa mashabiki, viongozi na wanachama wa Wekundu wa Msimbazi kwa kushirikiana pamoja kuanzia mwanzo wa msimu hadi mwisho wa safari yao ya kufunga msimu.

"Tuliianza safari pamoja, hawakutuacha, ninaamini tutaendelea pamoja katika kumalizia msimu kwenye mashindano ya Kombe la FA yaliyoko mbele yetu," alisema kiungo huyo wa zamani wa Simba na Super Sport ya Afrika Kusini.

Mabingwa hao wamebakiza mechi nne ambazo ni dhidi ya Mbao, Alliance, Coastal Union na Polisi Tanzania itakayochezwa kwenye Uwanja wa Chuo cha Ushirika mjini Moshi, Kilimanjaro.

Kikosi cha Simba kilirejea jijini Dar es Salaam jana asubuhi na jioni ilitarajiwa kuanza maandalizi ya kuwakabili watani zao, Yanga katika mchezo wa hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la FA itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa.

Habari Kubwa