Matola: Sababu Lipuli kuchezea vichapo hizi

14May 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Matola: Sababu Lipuli kuchezea vichapo hizi

KOCHA wa Lipuli FC, Selemani Matola, amesema uzembe na hali ya kubweteka ulioonyeshwa na mabeki wake, ndio sababu kuu ya wao kupoteza mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo sasa inaelekea ukingoni.

KOCHA wa Lipuli FC, Selemani Matola.

 

Kauli hiyo ya Matola, nahodha na kiungo wa zamani wa Simba na Supersport ya Afrika Kusini, ilikuja baada ya kuchapwa mabao 3-0 na Mbeya City, katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Samora mkoani Iringa.

Ijumaa iliyopita Lipuli ilifungwa mabao 2-0 na Ruvu Shooting ya Pwani huku pia ikichapwa mabao 3-0 na Biashara United katika mchezo mwingine wa ligi hiyo uliochezwa kwenye Uwanja wa Karume mjini Musoma.

Matola aliliambia gazeti hili kuwa, baada ya kumaliza mechi ya Kombe la FA dhidi ya Yanga ambapo waliibuka na ushindi, wachezaji wake walionekana "kuridhika" na kucheza soka la kiwango cha chini na hivyo kupoteza mechi hizo za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha huyo alisema hajaridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa katika mchezo huo huku pia washambuliaji wake wakionekana kukosa umakini wanapopata nafasi za kufunga na kujiweka katika nafasi mbaya.

"Wamecheza kizembe sana, kizembe kabisa, naona wamebweteka tangu tulipopata ushindi katika mechi dhidi ya Yanga, nimeliona hili, tutalifanyia kazi ili turudi katika ubora wetu, bado ligi haijamalizika, tunahitaji kupata ushindi katika mechi zilizobaki," alisema Matola.

Lipuli FC imecheza mechi 35 na ina pointi 48 wakati katika msimamo wa ligi hiyo ambayo Simba ndio bingwa mtetezi, tayari African Lyon ya jijini Dar es Salaam yenye pointi 22 imeshashuka daraja.

Lakini pia Simba na Yanga ndizo zimebakia katika mbio za kuwania ubingwa ili kukata tiketi ya kushiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.

Habari Kubwa