Matumla ulingoni Februari 2

08Jan 2017
Mahmoud Zubeiry
Nipashe Jumapili
Matumla ulingoni Februari 2

BONDIA Mohammed Matumla anatarajiwa kupanda ulingoni Februari 2, mwaka huu katika Uwanja wa Ndani wa Taifa, Dar es Salaam kuzipiga na Mfaume Mfaume katika pambano lisilo la ubingwa la uzito wa Feather.

Mratibu wa pambano hilo, Jocktan Masasi alisema jana wakati wa kutambulisha pambano hilo kwamba mabondia wote wamesaini mkataba mbele ya mwanasheria tayari kuzipiga Februari 2, mwaka huu.

Masasi alisema pambano hilo litasimamiwa na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC) na litatanguliwa na mapambano mengine kadhaa.

“Tumeamua kuandaa pambano hilo ili kumaliza ubishi baina ya mabondia hawa wawili, ambao wana upinzani wa muda mrefu, nani zaidi kati yao,”alisema promota huyo.

Masasi alisema katika mapambano hayo ya utangulizi, Iddi Mkwela atapigana na Manyi Issa uzito wa Light, Meshack Mwankemwa atapambana na Ramadhani Shauri uzito Welter, Mohammed Swedi atazipiga na Haidari Mchenjo uzito wa Bantama na Ibrahimu Maokola atazipiga na Zumba Kukwe kutoka Kibaha uzito wa Middle.

Habari Kubwa