Mavugo aikimbiza Simba, MO kuichukua timu kesho

14Aug 2016
Na Mwandishi Wetu
Lete Raha
Mavugo aikimbiza Simba, MO kuichukua timu kesho

UONGOZI wa Simba SC umesema upo katika mbio kali za hatua za mwisho kumaliza suala la uhamisho wa mshambuliaji wao, Laudit Mavugo.

Katibu wa Simba, Patrick Kahemela, ndiye aliyelieleza Lete Raha taarifa hizo juzi jioni jijini Dar es Salaam.
“Tupo katika hatua za mwisho za kushughulikia uhamisho wa Mavugo, ili ahalalishwe kuichezea timu yetu mara moja,”alisema Kahemela.

Mavugo ametua Simba SC baada ya kumaliza mkataba wake na Vital’O ya kwao Burundi, lakini klabu hiyo imeibuka na kudai mshambuliaji huyo wa bado ana mwaka mmoja zaidi wa kuitumikia.

Vital’O inaitaka Simba SC mezani wazungumze biashara ya Mavugo, lakini Kahemele amesema: “Sisi hatuna suala la kuzungumza na Vital’O kuhusu Mavugo. Tunashughulikia uhamisho wake tu kwa wahusika.”

Pamoja na hayo, klabu ya Solidarity nayo imeibua madai ya kummiliki Mavugo na kuitaka Simba SC ikae nao mezani kuzungumzia uhamisho wake.

Mavugo leo anatarajiwa kuichezea mechi ya pili Simba itakapomenyana na URA ya Uganda Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mavugo alicheza vizuri katika mechi yake ya kwanza Uwanja wa Taifa Jumatatu wiki hii dhidi ya AFC Leopard ya Kenya, Simba SC ikishinda 4-0, naye akifunga bao moja kati ya hayo.

MO mezani na viongozi wa Simba kesho
Wakati huo huo, Uongozi wa klabu hiyo unatarajiwa kuwa na kikao na mfanyabiashara Mohamed ‘MO' Dewji’ kesho jijini Dar es Salaam kujadili mpango wake wa kutaka kununua asilimia 51 ya hisa za klabu kwa Sh. bilioni 20, zoezi ambalo litailazimu klabu hiyo kwanza kubadilisha katiba ili kuhamia kwenye mfumo wa kuuza hisa.

Kahemela alisema jana kwamba maandalizi yote ya kikao hicho yamekamilika na Kikao hicho kinatarajia kuja na majibu ya mchakato mzima wa kuekelea kwenye mabadiliko.

Katika maombi yake, Mtendaji Mkuu huyo wa Kampuni ya Mohamed Enterprises Tanzania Limited (MeTL), alisema kuwa atakaponunua hisa ailimia 51 atataka kuitoa klabu hiyo kwenye bajeti ya bilioni 1.2 kwa mwaka hadi bilioni 5.5.

Tajiri huyo anaamini kuwa mashabiki wa Simba wanahitaji mafanikio ya haraka, ameahidi kusajili vizuri, kuajiri kocha mzuri, na kuhakikisha Simba inapata mafanikio kimataifa.