Mavugo: 'Hakunaga' kama Simba kwangu

10Aug 2016
Na Mwandishi Wetu
Lete Raha
Mavugo: 'Hakunaga' kama Simba kwangu

MSHAMBULIAJI mpya wa Simba, Laudit Mavugo, amesema kwa sasa yupo katika timu nzuri zaidi maishani mwake.

Laudit Mavugo

Akizungumza na Lete Raha juzi baada ya kuisaidia Simba kushinda 4-0 dhidi ya AFC Leopard ya Kenya, Mavugo alisema amefurahia mwanzo mzuri katika timu hiyo yenye makazi yake mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam.

“Nimefurahi, nimekuwa na mwanzo mzuri katika timu, nimetokea benchi nimekwenda kufunga na zaidi timu imecheza vizuri sana, naweza kusema hii ni timu nzuri zaidi kwangu kuwahi kuchezea,”alisema.

Mavugo anayetokea Vital’O ya kwao, Burundi, alisema sasa anaelekeza nguvu zake katika kuisaidia timu ya Simba kushinda mataji. “Kwa ushirikiano na wachezaji wenzangu naamini tutaweza, tuna timu nzuri,”alisema.

Simba juzi ilisherehekea vema miaka 80 baada ya kuifunga AFC Leopard ya Kenya mabao 4-0 katika mchezo wa kirafiki uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mshambuliaji chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Ibrahim Ajibu aliendelea kumvutia kocha mpya, Mcameroon Joseph Omog baada ya kufunga mabao mawili, huku wachezaji wapya, Mrundi Laudit Mavugo na Shizza Kichuya wakifunga pia.

Hadi mapumziko, Simba walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Ajibu dakika ya 38 kwa shuti la umbali wa mita takriban 30 baada ya kupokea pasi ya kiungo Mkongo, Mussa Ndusha.

Mabadliko ya karibu nusu kikosi yaliyofanywa na kocha Omog, anayesaidiwa na Mganda Jackson Mayanja, katika kipindi cha pili yaliisaidia Simba kupata mabao matatu.

Ajibu alimalizia vizuri krosi ya Kichuya hivyo kuifungia Simba bao la pili dakika ya 56 na dakika 58 Jamal Mnyate akapoteza nafasi nzuri aliyotengenezewa na Mavungo.

Hata hivyo, Kichuya akawainua vitini mashabiki wa Simba walioongozwa na Rais wa klabu hiyo, Evans Aveva na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kufunga bao la tatu dakika ya 66, akimalizia krosi ya Mavugo.

Mavugo aliyejiunga na Simba mwishoni mwa wiki, akaifungia timu hiyo bao la nne dakika ya 82 akiunganisha krosi nzuri ya Kichuya, aliyekuwa nyota wa mchezo huo.

Habari Kubwa