Maxime :Tuko kamili kuikabili Yanga Taifa

08Mar 2018
Somoe Ng'itu
Nipashe
Maxime :Tuko kamili kuikabili Yanga Taifa

KOCHA Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime, amesema kuwa kikosi chake kiko tayari kuikabili Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayofanyika kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

KOCHA Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime.

Tayari kikosi cha Kagera Sugar amnacho hakiko vizuri msimu huu kimeshatua jijini kuwafuata mabingwa hao watetezi.

Akizungumza na gazeti hili jana, Maxime, alisema kuwa yuko tayari kwa mechi hiyo na wameahidi kupambana ili kutopoteza pointi kama walivyofanya katika mechi ya kwanza walipokuwa nyumbani kwao Bukoba.

Maxime aliongeza kuwa anajua mechi hiyo itakuwa ngumu huku Yanga ikiwa imetoka katika mchezo wa kimataifa wa Ligi ya Mabingwa Afrika huku wakichapwa mabao 2-1 wapinzani wao Township Rollers ya Afrika Kusini.

"Tunajua hatuna msimu mzuri safari hii, lakini tunaweza kufanya vizuri ugenini na mechi zilizobakia nyumbani, hatujataka tamaa na tunaamini nafasi bado tunayo ya kubadili upepo huu mbaya ambao unatuzungukia," Maxime alisema.

Aliongeza kuwa hata kwenye vita ya kuwania ubingwa, hakuna timu yenye uhakika wa kutwaa taji hilo linaloshikiliwa na Yanga ya Dar es Salaam.

Simba ndio vinara wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 16 ikiwa na pointi 46 ikifuatiwa na Yanga wenye pointi 40 na mabingwa wa Kombe la Mapinduzi Azam FC ambao wana pointi 38.