Mayanga aachiwa rungu la usajili Ruvu

06Aug 2020
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Mayanga aachiwa rungu la usajili Ruvu

KLABU ya Ruvu Shooting imesema haikurupuki kwenye usajili au kuangalia timu fulani inasajili sana, badala yake itasajili kwa matakwa ya benchi lao la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Salum Mayanga na si vinginevyo.

Ofisa Habari wa klabu hiyo Masau Bwire alisema jana kuwa wao kama Ruvu Shooting hakuna eneo ambalo hawaliheshimu kama la usajili, ambalo halitakiwi kufanyiwa utani au kujaribu wachezaji.

Masau alisema hayo alipokuwa akielezea mustakabali wa klabu hiyo baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

"Eneo ambalo halitakiwi kufanyiwa utani ni eneo la usajili, kwa sababu ukikosea tu basi utalia msimu mzima. Kwa hiyo tuko makini katika hili na tutasajili kwa kufuata maelekezo ya mwalimu kwa sababu yeye ndiye anajua kikosi chake kilikuwaje, kibadilike vipi na nani asajiliwe, nani atoke," alisema msemaji huyo wa Ruvu Shooting na kuongeza.

"Kikosi kizuri cha soka kinaimarishwa na usajili mzuri, sisi hatukurupuki, au kuangalia fulani amefanya nini. Lakini kama kuna mchezaji atataka kuondoka sisi hatumzuii kwa sababu vijana maisha yao ni mpira, akiona anahitajika sehemu nyingine sisi huwa hatuna kinyongo ingawa jinsi wachezaji wetu wanavyolelewa na kuthaminiwa, sidhani kama wanaweza kukubali kuondoka haraka haraka hivi." alisema.

Kuhusu kocha Mayanga, Bwire amesema kuwa kocha huyo ameonyesha dhamira ya kubaki na timu hiyo, lakini uongozi wa Ruvu Shooting pia umeonyesha nia ya kumbakisha.

Habari Kubwa