Mayanga mbioni kujiunga na KMC

17Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR
Nipashe
Mayanga mbioni kujiunga na KMC

ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Salum Mayanga, anatarajiwa kutua katika kikosi cha KMC FC kurithi mikoba iliyoachwa na Mrundi Etienne Ndayiragije, ambaye tayari ametangazwa kujiunga na Azam FC, zote za jijini Dar es Salaam, imefahamika.

ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Salum Mayanga.

Mayanga msimu uliomalizika alikuwa akiifundisha Mbao FC ya jijini Mwanza ambayo inashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Taarifa zilizopatikana jana jijini zinaeleza kuwa uongozi wa KMC umeanza mazungumzo na Mayanga baada ya kushindwa kufikia makubaliano na Selemani Matola, ambaye jana alisaini mkataba rasmi wa kuitumikia Polisi Tanzania.

"Tayari ameshaanza mazungumzo na mambo yakienda vema, Mayanga atakuwa kocha mpya wa KMC, tunaamini tutamaliza majadiliano vizuri," alisema kiongozi mmoja wa KMC.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa wameanza kwanza kuboresha benchi la ufundi, ili kumpa nafasi kocha huyo mpya aweze kusajili wachezaji anaowataka na anaoamini watamsaidia katika msimu ujao.

Timu nyingine ambazo Mayanga amewahi kufanya nazo kazi hapa nchini ni Mtibwa Sugar ya Manungu, Turiani mkoani Morogoro na Tanzania Prisons ya jijini Mbeya.

Klabu zote zinazotarajiwa kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao zimeshaanza kuboresha vikosi pamoja na mabenchi ya ufundi kwa lengo la kujiandaa kuonyesha ushindani katika ligi hiyo na mashindano mengine watakayoshiriki.

Habari Kubwa