Mayanja aagiza Simba 'imlime' barua Kiiza

04Mar 2016
Sanula Athanas
Dar
Nipashe
Mayanja aagiza Simba 'imlime' barua Kiiza
  • Straika huyo wa kimataifa kutoka Uganda ameponzwa na ujumbe wake wa kumtetea Hassa Isihaka kwenye mtandao wa kijamii.

KATIKA kile kinachoonekana hana uvumilivu na watovu wa nidhamu, kocha wa muda wa Simba, Jackson Mayanja, ameuagiza uongozi wa klabu hiyo umlime barua ya onyo Hamis Kiiza kutokana na straika huyo kumtetea Hassan Isihaka aliyesimamishwa Msimbazi.

kocha wa Simba, Jackson Mayanja.

Jumatatu uongozi wa Simba ulitangaza kumfungia kwa muda usiojulikana Isihaha kwa madai kuwa beki huyo wa kati mwenye umri wa miaka 21 alitoa lugha chafu dhidi ya Mayanja.

Na katika kile kilichoonekana hakufurahishwa na uamuzi huo, Kiiza (25) aliandika kwenye mtandao wa kijamii akisikitika kumkosa Isihaka ambaye alidai ni mtu wake wa karibu.

"Ninampenda sana kijana huyu, ni mchezaji anayeongoza kwa nidhamu, mara nyingi nimekuwa naye.. haya mambo ya kuharibia jina la mtu, si vizuri. 'Nimekumiss' (nimekumbuka) nahodha wangu, nakupenda lakini Mungu yupo," Kiiza aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Ujumbe wa straika huyo wa kimataifa anayeongoza chati ya wafumani nyavu hatari msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na magoli 16 baada ya mechi 20, ulimchukiza Mayanja na kuiagiza klabu hiyo ya Msimbazi ichukue hatua za kinidhamu dhidi ya Mganda mwenzake.

"Kocha (Mayanja) hakufurahishwa na kitendo cha Kiiza," Haji Manara, msemaji wa Simba alisema jana. "Alikutana naye, mchezaji (Kiiza) akaomba radhi, lakini Mayanja amesema suala hilo lisiishie hapo, ameuagiza uongozi wa Simba Sports Club umwandikie barua ya onyo kali Kiiza.

"Hii mitandao ya jamii ina matatizo, watumiaji wake wamekuwa wakitawaliwa na mihemko na kujikuta wanaandika mambo ambayo mwisho wa siku yanawafedhehesha mbele ya jamii.

"Klabu ya Simba itaendelea kusimamia nidhamu ya wachezaji na viongozi wake wote. Ikumbukwe kuwa moja ya sababu za kumwondoa (Dylan) Kerr ilikuwa ni nidhamu mbovu ya timu. Nidhamu ya wachezaji wa Simba ilishuka kwa kiasi kikubwa."

Hii si mara ya kwanza kwa Simba kuchukua hatua ya kuwafungia na kuwaonya nyota wao. Msimu uliopita mabingwa hao mara 18 wa Tanzania Bara waliwafungia viungo Shaan Kisiga, Amri Kiemba na Haroun Chanongo kwa madai ya utovu wa nidhamu muda mfupi baada ya timu yao kulazimishwa sare ya 1-1 na Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya siku ya kwanza ya mwezi Novemba 2014.

Habari Kubwa