Mayanja asubiri mkataba Ihefu FC

16Oct 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Mayanja asubiri mkataba Ihefu FC

ALIYEKUWA Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, amesema bado hajasaini mkataba na uongozi wa Ihefu FC, lakini amekiri kufanya mazungumzo na klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mayanja ametoa kauli hiyo baada ya kuwapo kwa tetesi kwamba amesaini mkataba wa mwaka mmoja wa kukinoa kikosi cha timu hiyo ya jijini, Mbeya.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mayanja alisema kwa sasa yupo kwao Uganda, lakini klabu hiyo inakaribia kukamilisha mazungumzo ya kumwajiri kupitia kwa meneja wake.

Mayanja alisema mazungumzo yanaendelea vema na endapo mipango itakamilika, atarejea nchini kwa mara nyingine na kuiongoza timu hiyo iliyopanda daraja msimu huu.

“Hizi taarifa za kusaini mkataba hazina ukweli wowote, sababu mimi niko Uganda ila kuna mtu wangu wa karibu aliniambia juu ya malengo ya uongozi wa timu hiyo, nipo tayari kurejea Tanzania,” alisema Mayanja.

Taarifa zilizopatikana jijini jana zinasema mabosi wa timu hiyo wanasubiri kauli ya mwisho ya mmiliki wa timu hiyo, ambaye kwa sasa yupo nje ya nchi na atakaporejea, atalimaliza suala hilo.

Ihefu ilitangaza kumfukuza kazi aliyekuwa kocha wake, Maka Andrew, ambaye aliipandisha timu hiyo baada ya kupata matokeo mabaya katika mechi tano zilizopita za ligi hiyo.

Habari Kubwa