Mayanja atamba kuipiga Yanga 3-0, Pluijm…

17Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
Lete Raha
Mayanja atamba kuipiga Yanga 3-0, Pluijm…

MIAMBA ya soka nchini, Simba SC na Yanga inatarajiwa kukutana Jumamosi katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku makocha wa timu zote wakijiamini kupata matokeo mazuri.

YANGA

Mchezo wa kwanza Septemba 26, mwaka jana mabao ya Amissi Tambwe kipindi cha kwanza na Malimi Busungu kipindi cha pili yalitosha kuipa Yanga ushindi wa 2-0 dhdii ya watani wao hao wa jadi Uwanja wa Taifa.

Na mwishoni mwa wiki, Wekundu wa Msimbazi wataingia uwanjani wakiwa na deni hilo, huku kocha mpya wa timu hiyo, Mganda Jackson Mayanja akitamba kuwafunga 3-0 wapinzani.

Kiungo huyo wa zamani wa kimataifa wa Uganda, aliyejiunga na Simba SC katikati ya Januari baada ya kuondolewa kwa Muingereza, Dylan Kerr ameiambia Lete Raha kwamba amekuwa akiifuatilia Yanga inayofundishwa na Mholanzi, Hans van der Pluijm kwa muda mrefu, hususan kwenye michezo yao mitano iliyopita ya Ligi Kuu na haoni kwa nini asiwafunge Jumamosi.

Mayanja aliyeiongoza Simba kushinda mechi zote sita za Ligi Kuu tangu atue Msimbazi akitokea Coastal Union ya Tanga, amesema kwamba anatambua umuhimu wa kushinda mchezo huo na anaamini itakuwa rahisi kwake kutimiza malengo hayo, iwapo wapinzani watacheza mfumo wao ule ule uliozoeleka wa 4-3-3.

“Sitaki kuonekana kwamba ninaleta maneno mengi, bali ninachokueleza ndiyo ukweli. Nimeisoma mifumo anayoitumia Pluijm Yanga na nimejaribu kutafuta mbinu za kutegua mbinu zake anazotumia.

Pluijm kwenye michezo mingi amekuwa akitumia mfumo wa 4-3-3, ambao ni mfumo unaohitaji washambuliaji watatu wenye kuweza kucheza kitimu, lazima wawe na uwezo binafsi utakaowawezesha kuibeba timu inapozidiwa,”amesema kocha huyo wa zamani wa Kagera Sugar.

Mayanja ambaye enzi zake alichezea SC Villa na KCCA za kwao Uganda, amesema hana uhakika kama washambuliaji watatu wa Yanga SC, Mzimbabwe Donald Dombo Ngoma, Amissi Joselyn Tambwe na Simon Happygod Msuva wanaweza kucheza mfumo huo ipasavayo. “Kama amekuwa akipata matokeo (mazuri) kwa mfumo huo, basi ni dhidi ya timu dhaifu na siyo Simba yangu,” amesema.

“Bila kuwa na mfumo unaoendana na wachezaji wako ni kazi bure, kama Yanga wakiamua kutumia mifumo ambayo wamekuwa wakiitumia siku zote, basi kwangu nafakiri itakuwa sherehe. Ninaweza kutamba mapema nitawafunga hata mabao 3-0,” amesema.

Kwa upande wake, kocha wa Yanga, Pluijm pamoja amesema kwamba anawajenga wachezaji wake kisaikolojia waondokane na presha ya mechi hiyo.

“Kuna presha kubwa kwetu kutokana na ubora wa Simba kwa sasa, Simba ni timu nzuri na imekuwa na maendeleo mazuri kwa kipindi hiki na kikosi chake kimekuwa kikitoa ushindani mkubwa kwa timu nyingine kuliko nilivyokuwa nimeizoea, lakini sisi tutapigana ili tuweze kufanya vizuri,”amesema kocha huyo wa zamani wa Berekum Chelsea ya Ghana.

Pluijm amesema ni pigo kwake kumkosa beki wake tegemeo wa kati, Kevin Yondan anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu, lakini hana wasiwasi, kwani ana wachezaji wengine wa kucheza nafasi hiyo, akiwemo Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliyekuwa majeruhi kwa muda mrefu.

“Yondan hatakuwepo kwa sababu anatumia adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa dhidi ya Coastal Union. Bahati nzuri, Nahodha Cannavaro aliyekuwa nje kwa muda mrefu akisumbuliwa na maumivu amerudi na anaendelea vizuri na mazoezi kwa wiki sasa.

Sijui kama atakuwa fiti kucheza, nitajua Ijumaa. Na kwa ujumla hadi kufika Ijumaa nitakuwa nimekwishajua mipango ya mechi imekaaje,” amesema.

Pluijm hakutaka kuuzungumzia sana mchezo, zaidi ya kusema wapizani wake wako vizuri safari hii na anatarajiwa mchezo mgumu Jumamosi.

VIKOSI;

Kocha Mayanja amefanya mabadiliko kidogo katika kikosi cha kwanza cha Simba kutoka kile cha Kerr, akiwarudisha benchi kipa Peter Manyika, beki Hassan Isihaka na kiungo Said Ndemla na sasa anawatumia zaidi langoni Vincent Angban kutoka Ivory Coast, Abdi Banda katika beki ya kati na Jonas Mkude kama kiungo mchezeshaji.

Aidha, Mayanja pia amemuingiza kwenye kikosi cha kwanza beki Mrundi, Emery Nimubona, huku Hassan Kessy mara kadhaa akimchezesha mbele kulia.

Katika mchezo wa Jumamosi hayatarajiwi mabadiliko kwenye kikosi cha Mayanja, labda Nimubona anaweza kuanzia benchi, ili Kessy acheze beki ya kulia na kushoto acheze Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, wakati mabeki wa kati wanaweza kuwa wale wale, Abdi Banda na Mganda Juuko Murshid.

Viungo wanatarajiwa kuwa Justice Majabvi chini, juu Jonas Mkude wakati viungo wa pembeni wanatarajiwa kuwa Mwinyi Kazimoto na Peter Mwalyanzi huku Ibrahim Hajib na Hamisi Kiiza wakiendelea kucheza pamoja katika safu ya ushambuliaji.

Yanga SC bila shaka Ally Mustafa ‘Barthez’ ataendelea kusimama langoni Jumamosi, beki wa kulia Juma Abdul, kushoto Oscar Joshua kama Mwinyi Mngwali atakuwa bado hajapona, wakati katikati wanaweza kucheza Mbuyu Twite na Vincent Bossou kama Cannavaro atakuwa bado hajawa fiti kucheza.

Viungo wanaweza kuwa Thabani Kamusoko na Haruna Niyonzima katikati, wakati pembeni wanaweza kuanza Deus Kaseke na Simon Msuva na washambuliaji Amissi Tambwe na Donald Ngoma.

Kama Cannavaro atakuwa tayari kurejea, maana yake Pluijm atatafuta sehemu nyingine ya kumtumia ‘fundi’ Twite anayeweza kucheza nafasi zote uwanjani kasoro kipa.

MECHI TANO ZILIZOPITA

Yanga SC katika mechi tano za Ligi Kuu zilizopita, imeshinda tatu dhidi ya Ndanda 1-0, Majimaji 5-0 na JKT Ruvu 4-0, nyingine ikitoa sare ya 2-2 na Prisons na moja kufungwa 2-0 na Coastal Union.

Simba SC imeshinda zake zote tano zilizopita 2-0 dhidi ya JKT Ruvu, 4-0 dhidi ya African Sports, 5-1 dhidi ya Mgambo JKT, 1-0 Kagera Sugar na 2-1 Stand United.

Matokeo hayo yalitosha kuipandisha Simba SC kileleni mwa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu, wakifikisha pointi 45 sasa baada ya kucheza mechi 19, mbili zaidi ya mahasimu wao, Yanga SC waliocheza mechi 18.

Jumla ya mechi 12 za watani wa jadi, zimechezwa tangu mwaka 2010 katika Ligi Kuu, Yanga SC wakishinda nne, Simba SC tatu, wakati tano zilimalizika kwa sare.

Simba SC inajivunia kuvuna mabao 15 ndani ya mechi hizo, huku mahasimu wao wakifunga mabao 14 licha ya kuongoza kushinda idadi ya mechi.