Mayanja: Inaniuma Simba kuboronga

13May 2016
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Mayanja: Inaniuma Simba kuboronga

KOCHA wa Simba, Jackson Mayanja, amesema kuwa anahuzunishwa kuona kikosi chake kikimaliza vibaya mechi za Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara huku tayari kikiwa kimeshapoteza ubingwa wa ligi hiyo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mayanja alisema kuwa mipango yake ilikuwa ni kuona Simba inafanya vizuri na kutimiza ndoto za kutwaa ubingwa huo uliokosekana kwa miaka misimu minne.

Mayanja alisema kuwa kama kikosi hicho kingeendelea na kasi aliyoanza nayo, wangetwaa ubingwa huo na kumaliza 'machungu' waliyonayo wanachama na mashabiki wa timu hiyo.

"Sijafanya vibaya sana, lakini nilikuwa na mwanzo mzuri na mipango yangu ilikuwa kumaliza vizuri ligi kuu..., lakini huu ndio mpira ulivyo," alisema Mayanja.

Alisema kuwa matokeo hayo ambayo Simba imepata anayakubali na kueleza kuwa ni sawa na 'ajali' kwenye soka.

Simba imebakiza mechi mbili za ligi ambazo ni dhidi ya Mtibwa Sugar itakayofanyika Jumapili mkoani Morogoro na JKT Ruvu ambayo itakuwa ya mwisho msimu huu.

Habari Kubwa