Mayanja 'kuiua' Yanga kwa mifumo

07Feb 2016
Lete Raha
Mayanja 'kuiua' Yanga kwa mifumo

HII ni hatari kwa Yanga. Simba inayopikwa na kocha raia wa Uganda, Jackson Mayanja, imepania kutoa kipigo cha maana. Kocha huyo anawatengeneza wachezaji wake waweze kucheza kwa dakika 120 bila kuchoka huku akiwa tayari anafanya majaribio ya mifumo mitatu tofauti kwaajili ya kuifunga Yanga.

Kocha huyo wa zamani wa Kagera Sugar ameanza kwa kishindo akiiongoza Simba kushinda mechi tano zilizopita katika michuano yote (kabla ya mechi ya jana dhidi ya Kagera Sugar) tangu arithi mikoba Muingereza Dylan Kerr aliyetimuliwa Msimbazi.
Alishinda 1-0 dhidi ya Mtibwa, 2-0 dhidi ya JKT Ruvu, 3-0 dhidi ya Burkina Faso, 4-0 dhidi ya African Sports na 5-1 dhidi ya Mgambo JKT na hivyo kuanzisha utani kwamba wangeendelea kushinda goli moja zaidi kwa kila anayekuja mbele yao.
Imefahamika kuwa kocha huyo alipokuwa Kagera alimudu kuzifunga Simba na Yanga dhidi yake kwa kutumia mifumo mitatu tofauti ambayo ilikuwa ikihusisha pasi nyingi fupifupi. Pia kocha huyo alitumia zaidi ubunifu wa wachezaji ikiwamo uwezo wa kupiga pasi nyingi na kuwakimbiza kwa muda mrefu bila kuchoka.
Aliyewahi kuwa msaidizi wa Mayanja kwa zaidi ya miaka mitano kwenye klabu ya Kagera Sugar, Mrange Kabange, alisema, “Nimemfahamu Mayanja kwa muda mrefu tukiwa Kagera. Ni kocha anayependa timu yake iwe na uwezo wa kucheza kwa dakika 120 kwa kasi bila kuchoka. Pia anapenda timu yake icheze mpira wa pasi nyingi, lakini pia anapenda wachezaji wawe wabunifu.
“Kimsingi tulizishinda Simba na Yanga kutokana na mifumo tuliyokuwa tukiitumia. Tulichanganya mifumo mitatu kwenye mchezo mmoja kwa kuangalia mahitaji yetu kwenye kila dakika za mechi.
“Mfano tulicheza sana kwa mifumo ya 4-3-3, 4-4-2 na 3-5-2.
4-4-2 ni mfumo unaokuwa na mabeki wanne, viungo wanne na washambuliaji wawili, wakati 4-3-3 ni mfumo ambao una mabeki wanne, viungo watatu na washambuliaji watatu. Mfumo mwingine ni ule wa 3-5-2 ambao hujaza viungo. Mfumo huo huwa una mabeki watatu nyuma, viungo watano katikati na washambuliaji wawili mbele.
Kulingana na staili hiyo ya ufundishaji ya Mayanja, Kabange alisema kuwa kama Simba itacheza na Yanga kisha Mayanja akafanikiwa kuifanya timu yake kutawala mpira basi Yanga wanakuwa wamekufa moja kwa moja.
Alisema, “Mayanja akishakusoma kisha akatawala mchezo basi ndiyo mwisho wako. Kwa jinsi ninavyomfahamu Mayanja sijui kama Yanga watatoka kwenye mchezo huo.
Naye Mayanja alisema, “Nilikuta stamina ya wachezaji Simba ipo chini. Wengi hawakuwa fiti, lakini sasa taratibu ninawatengenezea uwezo wa kumudu kucheza bila kuchoka kwa dakika 90, naamini mpaka mchezo wetu na Yanga watakuwa fiti na nitajua nitatumia mfumo gani wa kuifunga Yanga.”
Joto la mchezo kati ya Simba na Yanga linaendelea kuwa kali huku klabu hizo zote zikiwa na michezo miwili kila timu kabla ya kukutana na mahasimu wao.

Habari Kubwa