Mayanja: Yanga kipigo chenu kimeiva

14Feb 2016
WAANDISHI WETU
Nipashe Jumapili
Mayanja: Yanga kipigo chenu kimeiva

SIMBA jana ilikwea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Kuu Bara kwa mara ya kwanza msimu, huku Kocha Jackson Mayanja akitamba: "Lazima Yanga wafungwe Jumamosi ijayo."

Wachezaji wa timu ya Simba

Magoli mawili ya straika Hamis Kiiza yalimpa kocha huyo ushindi wa 2-1 dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga ikiwa ni mara ya sita mfululizo kikosi cha Simba chini ya Mganda huyo kinatoka kifua mbele Ligi Kuu.

"Nimefurahi kuona tumefanikisha lengo letu la kupata pointi sita hapa (Shinyanga)," alisema Mayanja. "Ushindi huu ni muhimu kwetu, unatupa nguvu ya kuikabili Yanga tukiwa na ari. Tunapaswa kushinda mechi ijayo...naamini tutashinda dhidi ya Yanga."

Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 45 baada ya mechi 19, pointi mbili mbele ya Yanga wanaokamata nafasi ya pili.

Tangu msimu wa 2012/13 ambao Yanga walitwaa ubingwa licha ya kuanza vibaya kwa kutoka suluhu jijini Mbeya dhidi ya Prisons kabla ya kupoteza ugenini 3-0 na 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar na Kagera Sugar, timu hiyo ya Msimbazi ilikuwa haijawahi kusimama kileleni.

Azam FC, Mtibwa Sugar, Yanga na Ndanda FC ndizo timu pekee ambazo kwa nyakati tofauti ziliwahi kuongoza ligi.
Simba itaendelea kukaa kileleni ikiwa Azam FC watashindwa kuibuka na ushindi wa kuanzia magoli 3-1 watakapoikabili Coastal Union, Tanga leo jioni.

Dakika nne baada ya nusu saa ya mchezo, akiwa nje kidogo mwa boksi, mshambuliaji Kiiza aliifungia Simba goli lililodumu kipindi kwanza akimalizia kwa shuti kali la mguu wa kulia pasi ya straika aliye katika kiwango, Ibrahim Ajibu.

Lilikuwa bao la 15 kwa Mganda huyo lililomfanya aongoze chati ya wafumania nyavu akimuacha kwa goli moja Mfungaji Bora wa VPL 2013/14, Mrundi Amissi Tambwe wa Yanga.

Kama ilivyokuwa katika mechi ya Mwadui FC dhidi ya Simba mjini hapa Desemba 26 mwaka jana, mara tu baada ya kupulizwa kwa kipenga cha mwisho kipindi cha kwanza, kulinyesha mvua mjini hapa.

Kabla ya mvua hiyo kuongezeka na kuharibu ladha ya soka mjini hapa, Kiiza alitumia dakika mbili tu za kipindi cha pili kuandikisha goli la 16 kwake msimu huu na la pili kwa timu yake akimalizia kwa kichwa krosi ya beki Hassan Kessy.

Kiiza alipata nafasi nzuri ya kupiga 'hat-tick' ya pili msimu huu, lakini shuti lake la mguu wa kulia liligonga mwamba katika dakika ya 87.

Dakika mbili baadaye, straika 'kinda' Pastori Athanas aliwafuta machozi Stand United akitumia mwanya wa makosa ya beki Mrundi Emery Nimubona.

MATOKEO MENGINE
Mgambo JKT 0 - 1 African Sports
Mbeya City 5 - 1 Toto Africans
JKT Ruvu 1 - 1 Kagera Sugar
Imeandikwa na Sanula Athanas, Lasteck Alfred (Shinyanga) na Juma Mohamed (Mtwara)

Habari Kubwa