Mayanja: Yanga wazuri, lakini Simba hii kiboko

18Feb 2016
Sanula Athanas
Nipashe
Mayanja: Yanga wazuri, lakini Simba hii kiboko

KOCHA wa Simba, Jackson Manyanga, amesema itafanya vizuri dhidi ya Yanga katika mechi ya keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa kutokana na kuimarika kwa kikosi chake.

Timu hizo zitachuana katika mechi hiyo ya pili ya watani wa jadi msimu huu itakayochezeshwa na refa mwanamama Jonesia Rukyaa kutoka Kagera.

Akiwa kambini Morogoro jana mchana, Mganda huyo aliiambia Nipashe kuwa kutokana na kiwango kizuri cha wachezaji, kujitoa pamoja na morali yao, anaamini watapata ushindi dhidi ya mabingwa haoi watetezi.

Alisema timu yake haitarajii kitu kingine zaidi ya ushindi katika mechi ambayo ndiyo itatoa dira ya timu itakayotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu.

“Wachezaji wetu wako tayari kwa mechi ya watani, Yanga ni timu nzuri yenye wachezaji wazuri na wenye uzoefu na kucheza dhidi yao mara zote ni mechi ngumu, lakini tuko tayari kuwakabili wikendi hii,” alisema.

YANGA WALONGA

Wakati Mayanja akitoa tambo hizo, kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, alisema jana kuwa hawaoni sababu kuntu kwa kikosi chao kupoteza mechi ya Jumamosi kutokana na maandalizi mazuri wanayoendelea kuyafanya visiwani Pemba pamoja na kurejea uwanjani kwa nyota wao waliokuwa majeruhi.

Mwambusi, kocha wa zamani wa Mbeya City FC, alisema anajua mechi itakuwa mgumu kutokana na ubora wa kikosi cha Simba ambacho kimeshinda mechi zote saba zilizopita za VPL
(sita chini ya Mayanja).

“Tunakijua kile ambacho kinawapa matumaini ya kushinda mchezo wa Jumamosi, lakini tumejipanga kuepukana nacho na kushinda kama ilivyokuwa mzunguko wa kwanza. Tutaonyesha ubora wetu siku hiyo uwanjani,” alisema Mwambusi.

Takwimu za Nipashe zinaonyesha kuwa katika mechi 12 zilizopita za watani wa jadi Ligi Kuu tangu mwaka 2010, Simba inayoongoza msimamo wa VPL kwa sasa ikiwa na mtaji wa pointi 45, imefunga mabao 15 dhidi ya Yanga, lakini Wanajangwani wameshinda mara nne huku wapinzani wao wakiibuka na ushindi mara tatu.

Ushindani mwingine mkali unaosubiriwa Jumamosi utawahusisha kinara wa Hamis Kiiza wa Simba na Amissi Tambwe wa Yanga wanaowania kiti cha Simon Msuva cha Mfungaji Bora wa msimu.

Kiiza ametupia mara 16 katika mechi 19 ambazo Simba imecheza msimu huu wakati Tambwe yuko nyuma ya Mganda huyo kwa mabao mawili.

12 ZILIZOPITA SIMBA vs YANGA VPL
1. Simba 4-3 Yanga (Aprili 18, 2010)
2. Yanga 1-0 Simba (Okt 16, 2010)
3. Simba 1-1 Yanga (Machi 5, 2011)
4. Yanga 1-0 Simba (Okt 29, 2011)
5. Simba 5-0 Yanga (Mei 6, 2012)
6. Simba 1-1 Yanga (Okt 3, 2012)
7. Yanga 2-0 Simba (Mei 18, 2013)
8. Yanga 3-3 Simba (Okt 20, 2013)
9. Simba 1-1 Yanga (Aprili 19, 2014)
10. Simba 0-0 Yanga (Okt 18, 2014)
11. Simba 1-0 Yanga (Machi 8, 2015)
12. Yanga 2-0 Simba (Sept 26, 2015)