Mbao FC wataka mafanikio zaidi

22Oct 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Mbao FC wataka mafanikio zaidi

UONGOZI wa timu ya soka ya Mbao FC ya jijini Mwanza, umesema kuwa umejipanga kupata mafanikio zaidi ya yale waliyopata msimu uliopita ambao walipanda daraja na kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa Mbao FC, Solly Njoshi, alisema kuwa udhamini waliopata kutoka kwa makampuni tofauti umewaongezea nguvu ya kupambana kwenye ligi na mashindano ya Kombe la FA watakayoshiriki.

Njoshi alisema kuwa ligi msimu huu ni ngumu zaidi na ili timu iweze kufanya vizuri, ni lazima klabu iwe na nguvu ndani na nje ya uwanja.

"Mwaka jana tulikuwa na malengo yetu yalikuwa ni kuhakikisha tunapambana ili tubaki Ligi Kuu na kwenye mashindano ya Kombe la FA, kwa sababu pia tulikuwa wageni, tulisema tunataka tufike robo fainali, lakini tulivuka mpaka tukacheza fainali," alisema mwenyekiti huyo.

Aliongeza kuwa wanawashukuru mashabiki wa ndani na nje ya Mwanza kwa kuwapa ushirikiano bila kumsahau mlezi wao ambaye ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angella Mabula.

Baada ya kumaliza mechi dhidi ya Azam FC, kikosi cha timu hiyo ya Mbao FC kitasafiri kwenda Iringa kuifata Lipuli FC halafu itaelekea Njombe kucheza na wenyeji wao Njombe Mji.

Habari Kubwa