Mbao zaiangukia  Yanga Kirumba 

01Jan 2018
Faustine Feliciane
Nipashe
Mbao zaiangukia  Yanga Kirumba 
  • ***Zavunja rekodi yao ya kutopoteza Ligi Kuu, Kayombo akimtafuta Okwi ufungaji...

HATIMAYE Mbao FC imeendeleza rekodi yake ya kuitungua Yanga kwenye Uwanja wa CCM Kirumba baada ya kuitandika kwa mabao mawili 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa jana uwanjani hapo.

Tangu Mbao FC imepanda Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza msimu uliopita, Yanga haijawahi kuifunga katika Uwanja wa CCM Kirumba ikiwa ni pamoja na kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho.

Kadhalika, kwa ushindi huo wa jana Mbao inakuwa timu ya kwanza kuifunga Yanga kwenye mechi za Ligi Kuu msimu huu, hivyo kukifanya kikosi hicho cha Mzambia George Lwandamina kubaki na pointi zao 21 katika nafasi ya tatu kikiwa sawa na Mtibwa Sugar. 

Kipigo hicho kinawafanya mashabiki wa Yanga kuunza mwaka mpya vibaya huku pia wakikubali kuwa nyuma ya watani zao Simba kwa pointi tano.

Ushindi wa jana ni watatu kwa  Mbao dhidi ya Yanga kwenye uwanja huo huku kipigo cha kwanza kikiwa kwenye nusu fainali ya Kombe la FA ambapo walishinda 1-0 kabla Mei 20, mwaka jana kwenye mchezo wa kufunga pazia Ligi Kuu msimu uliopita Mbao kuchomoza tena kwa  ushindi wa bao 1-0.

Katika mchezo wa jana, mshambuliaji Habibu Kayombo, alikuwa mwiba mkali kwa Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, baada ya kufunga mabao yote mawili kwenye kipindi cha pili cha mchezo huo.

Kayombo, alianza kuiipatia Mbao bao la kwanza katika dakika ya 52 baada ya kuachia shuti la 'Mama mkanye Mwanao' akiwa katikati ya uwanja na kumshinda kipa Youthe Rostand.

Kayombo ambaye jana alikuwa kwenye kiwango cha juu, alitumia mtindo uleule kuipatia timu yake bao la pili kwa guu la kushoto katika dakika ya 68.

Mabao hayo mawili yanamfanya kumpiku kwenye ufungaji mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa baada ya kufikisha mabao saba moja zaidi ya Chirwa na sasa anazidiwa bao moja tu na kinara Emmanuel Okwi wa Simba.

Katika mchezo wa jana, Yanga ambayo iliwakosa nyota wake, Chirwa, Ibrahim Ajibu na Kelvin Yondani, haikucheza kwenye kiwango chake cha juu huku pia Mbao FC wakipata pigo katika dakika ya 75 baada ya beki wake Davis Mwasa kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Seleman Kinugani kutoka Morogoro baada ya kumchezea vibaya Amissi Tambwe na kupewa kadi ya pili ya njano ikifuatiwa na nyekundu.

Lakini pia mwamuzi huyo alimtoa kwenye benchi kocha wa Mbao FC, Etienne Ndayiragije na kumuamuru kwenda kukaa kwenye benchi kutokana na kumbugudhi mwamuzi msaidizi.

Yanga ilicharuka dakika 10 za mwisho kujaribu kusawazisha mabao hayo, lakini juhudi zao hazikuza matunda baada ya Pius Buswita kukosa bao dakika ya 84 huku pia mpira wa adhabu uliopigwa na mtokea benchi, Hassan Kessy aliyeingia kuchukua nafasi ya Juma Abdul, ukigonga mwamba kabla ya kuokolewa na mabeki wa Mbao.

Yanga jana haikuwa na Kocha wake Mkuu,  Lwandamina ambaye yupo kwao kwa matatizo ya kifamilia, hivyo timu hiyo kuongozwa na makocha wasaidizi, Shadrack Msajigwa.